1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi ulidhoofisha demokrasia Kenya - EU

11 Januari 2018

Uchaguzi wa urais wa Kenya uliokumbwa na visa vya udanganyifu uliidhoofisha demokrasia nchini humo na haya ni kulingana na waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/2qfr5
EU-Abgeordnete Marietje Schaake
Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa EU Marietje SchaakePicha: B. Belloni

Katika ripoti waliyoizindua hapo Jumatano ambayo imeughadhabisha upande wa serikali. Rais Uhuru Kenyatta alishinda uchaguzi wa marudio na kupata muhula wake wa pili baada ya ushindi wake wa awali kufutiliwa mbali na Mahakama ya Juu nchini humo.

Mkuu wa kikosi hicho cha uangalizi Marietje Schaake ambaye pia ni mbunge katika bunge la Ulaya amesema Wakenya walikuwa na matumaini makubwa, ila matumaini hayo yaligeuka na kuwa ya kufadhaisha. Schaake amesema Kenya inasalia kuwa nchi iliyogawika pakubwa.

Ripoti hiyo imesema kuwa mchakato wa upigaji kura uliharibiwa na hatua ya viongozi wa kisiasa kuzishambulia taasisi huru na pia kutokana na kutofanyika kwa mazungumzo baina ya pande mbili hasimu jambo lililochangia katika kuenea kwa mizozo na machafuko.

Umoja wa Ulaya umetoa mapendekezo kadhaa ili kuimarisha mchakato wa uchaguzi miaka ijayo

Waangalizi hao wanasema upande wa Rais Kenyatta uliitishia idara ya mahakama baada ya ushindi wake kufutiliwa mbali baada ya uchaguzi wa Agosti, huku upande wa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga ukiishambulia tume ya uchaguzi nchini humo mara kwa mara.

Kenia Oberstes Gericht annuliert Wahlen
Mahakama ya juu ilifutilia mbali uchaguzi wa AgostiPicha: picture-alliance/AP Photo/B. curtis

Ripoti hiyo ilitoa mapendekezo 29 yakiwemo mabadiliko ya kisheria na uchaguzi, Tume ya Uchaguzi kupewa nguvu zaidi na pia kuimarishwa kwa teknolojia, jambo litakalotoa nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi bora mwaka 2022 ambapo Kenyatta anatakiwa kuondoka madarakani.

Waangalizi hao pia walibaini matumizi mabaya ya rasilimali za taifa katika ngazi ya kitaifa na hata mashinani na kuwapa nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi wale waliokuwa madarakani kwa wakati huo.

Ripoti hiyo ilizinduliwa Brussels, Ubelgiji badala ya Kenya na Schaake anasema uongozi wa Kenya haukuwa tayari kumpokea yeye pamoja na kikosi chake kwa ajili ya uzinduzi wa ripoti hiyo wiki hii kama walivyokuwa wamepanga. Waangalizi hao wa Umoja wa Ulaya walishambuliwa na pande zote mbili, serikali na upinzani katika uchaguzi huo uliopita.

Balozi wa Kenya Ubelgiji amekanusha vikali madai ya Schaake

Lakini Balozi wa Kenya katika Umoja wa Ulaya na Ubelgiji Johnson Weru amekanusha madai ya Schaake na kusema kuwa ujumbe huo wa waangalizi ulikuwa umepanga kuzuru Kenya na kuzindua ripoti hiyo katikati ya mwezi Februari na Machi.

Kenia Wahlen 2017 Proteste
Kulishuhudiwa ghasia katika ngome kadhaa za upinzaniPicha: Reuters/B. Ratner

Katika taarifa, Weru amesema serikali ya Kenya inasikitishwa na jinsi waangalizi hao wa Umoja wa Ulaya walivyozindua ripoti yao ya mwisho kwa kutofuata mpangilio uliokuwepo.

Ripoti hiyo vile vile imesema Tume ya Uchaguzi ya Kenya ilifanya kazi yake vyema katika marudio ya uchaguzi wa Oktoba ikilinganishwa na jinsi ilivyosimamia uchaguzi wa Agosti, ingawa inadai hatua ya upinzani na wadau wengine kutoiamini tume hiyo, ni jambo lililochangia katika kuufanya mchakato mzima wa upigaji kura usionekane kwamba ulikuwa huru na wa haki.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/Reuters

Mhariri: Grace Patricia Kabogo