1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa bunge la Ulaya waingia siku ya pili

23 Mei 2014

Uchaguzi wa bunge la Ulaya unaendelea huku ukishuhudia chama cha UK Independence UKIP cha Uingereza, kikipata matokeo mazuri ambayo hayakutarajiwa hapo awali

https://p.dw.com/p/1C56p
Europawahl Großbritannien 22.05.2014
Picha: Lindsey Parnaby/AFP/Getty Images

Raia wa Ireland pamoja na Czech wanaingia siku ya pili ya upigaji kura wa bunge hilo. Kiongozi wa chama kinachopinga Umoja wa Ulaya na wahamiaji nchini Uingereza, UK independence, UKIP, Nigel Farage, amesema chama chake sasa kitauchukulia uchaguzi wa Bunge la Ulaya kwa umakini mkubwa.

Katika matokeo ya mabaraza 61 kati ya 161, UKIP kimefanikiwa kupata viti 89 ambapo katika uchaguzi wa awali kilipata kiti kimoja tu. Chama kikuu cha upinzani cha Uingereza, Labour, nacho kimepata viti 102, wakati chama cha Conservative kinachoongozwa na Waziri Mkuu David Cameron kikipoteza viti 97 huku Liberal Democratic kinachoongozwa na Naibu Waziri Mkuu Nick Clegg kikipoteza viti 99.

Chama cha UKIP kina matumaini ya kuongeza idadi ya wajumbe wake tisa katika bunge la ulaya wakati matokeo rasmi ya bara zima la ulaya yatakapotangazwa kesho kutwa usiku. Kiongozi wa chama cha UKIP Nigel Farage ameelezea matokeo hayo mazuri ya chama chake. Kwa mujibu wa makadirio ya awali, idadi ya wananchi wa uingereza waliojitokeza kuwapigia kura wawakilishi wao imeshuka hadi kufikia asilimia 36.

Kiongozi wa chama cha UKIP, Nigel Farage
Kiongozi wa chama cha UKIP, Nigel FaragePicha: Junge Alternative NRW

Kwingineko, wananchi wa Ireland na Czech wameingia siku ya pili ya zoezi la kupiga kura kuwachagua wajumbe wao watakaokuwepo katika bunge lijalo la Umoja wa Ulaya. Nchini Ireland vituo vya kupigia kura vilifunguliwa kuanzia saa moja asubuhi na vinatarajiwa kufungwa saa nne usiku, wakati Jamuhuri ya Czech wananchi wa nchi hiyo wanatarajia kuanza kupiga kura kuanzia saa nane mchana mpaka saa nne usiku. Chama cha upinzani cha nchi hiyo Ano, kinachoongozwa na billionea Adrej Babis kinatazamiwa kupata wingi wa viti katika uchaguzi huo huku chama ambacho kimeungana nacho kuunda serikali ya mseto cha CSSD kinatazamiwa kushika nafasi ya pili. Huko nchini Uholanzi chama kinachofuata siasa za mrengo wa kushoto cha nchi hiyo kinachoongozwa na Geert Wilders kimepigwa mweleka katika matokeo ya uchaguzi wa bunge la ulaya.

Chama hicho kinachopinga Kamisheni ya Ulaya pamoja na Uislamu kilitarajiwa kupata matokeo mazuri hapo awali lakini mambo yamekuwa ndivyo sivyo. "Matokeo yaliyotolewa yanakatisha tamaa, tunapigana kuelekea Brussels na kwa sasa tunaangalia chama ambacho tutashirikiana nacho" alisema Wilders.

Raia wa Ulaya wapatao 400 walikuwa wanatarajiwa kuwapigia kura wawakilishi wao katika bunge lijalo la Ulaya lakini maafisa wa uchaguzi huo wanaamini kuwa idadi hiyo itapungua kutokana na asilimia chache ya watu kujitokeza katika uchaguzi huo ambao matokeo yake rasmi yatatangazwa kesho kutwa usiku.

Mwandishi: Anuary Mkama/afpe, dpae
Mhariri: Mohammed Khelef