1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Libya kufanyika Juni

22 Mei 2014

Libya imeitisha uchaguzi hapo mwezi wa Juni kulichaguwa bunge la mpito lenye utata na kujaribu kutatuwa mzozo wa kuwania madaraka lakini ghasia miongoni mwa makundi ya wanamgambo zinatishia kuvuruga uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/1C40U
Waasi wa zamani waliojumuishwa katika jeshi la Libya wakiwa katika ulinzi Tripoli.
Waasi wa zamani waliojumuishwa katika jeshi la Libya wakiwa katika ulinzi Tripoli.Picha: AFP/Getty Images

Nchi yenye utajiri wa mafuta ya Libya imeitisha uchaguzi hapo mwezi wa Juni kulichaguwa bunge la mpito lenye utata na kujaribu kutatuwa mzozo wa kuwania madaraka lakini ghasia miongoni mwa makundi ya wanamgambo zinatishia kuvuruga uchaguzi huo. .

Ikionyesha uzito wa tishio la usalama,mnadhimu mkuu wa kikosi cha wanamaji nchini Libya Adimeri Hassan Abu Shnak, dereva wake na walinzi wawili wamejeruhiwa leo hii wakati watu wenye silaha walipoushambulia msafara wake mjini Tripoli.Haikuweza kujulikana mara moja kanali huyo aliejeruhiwa kidogo kichwani alikuwa na misimamo gani ya kisiasa na kipi kilichopelekea kushambuliwa kwake.

Wanamgambo wamekuwa wakilaumiwa kwa kuongezeka kwa machafuko katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini tokea uasi mwa mwaka 2011 ulioungwa mkono na mashambulizi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO ulipomuuwa aliekuwa kiongozi wa Libya wakati huo Moamer Gaddafi.

Serikali mbali mbali zilizoiongoza nchi hiyo zimelalamika kwamba madai ya Baraza Kuu la Taifa (GNC) kwamba lina madaraka ya utendaji kama bunge la kutunga sheria limezifunga mikono katika suala la kuwadhibiti wanamgambo.

Uchaguzi kufanyika Juni 25

Tume ya uchaguzi imesema uchaguzi wa bunge hilo la mpito ambalo hivi sasa linadhibitiwa na wajumbe wa itikadi kali za Kiislamu utafanyika Juni 25.Wakati baadhi ya waangalizi wana mashaka iwapo uchaguzi huo utaweza kufanyika mwandiplomasia mmoja wa nchi za magharibi ameliambia shirika la habari la AFP uchaguzi huo utafanyika na kwamba tume ya uchaguzi ina vifaa na rasilmali watu zinazohitajika kuandaa uchaguzi huo kwa wakati uliopangwa.

Generali muasi Khalifa Haftar.
Generali muasi Khalifa Haftar.Picha: Reuters

Serikali inataraji uchaguzi huo unaweza kusaidia kuepusha vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya generali muasi Khalifa Haftar ambaye serikali imemwita kuwa mvunja sheria kuwashambulia wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu hapo Ijumaa katika mji wa Benghazi.

Wapiganaji kutoka kundi la waasi wa zamani la kikosi cha Zintan wamesema wanamuunga mkono Haftar na kulivamia bunge hapo Jumapili ambapo walichoma moto jengo moja dogo lililopakana na jengo la bunge.

Haftar azidi kuungwa mkono

Haftar amekuwa akizidi kuungwa mkono katika kampeni yake ya kuwatokomeza wapiganaji wa jihadi nchini Libya.Wafuasi wake ni pamoja na kikosi maalum cha jeshi la taifa mjini Benghazi ambao walipata hasara kubwa katika mashambulizi yanayotuhumiwa kufanywa na majihadi katika mji huo wa mashariki ambapo wanamgambo wa itikadi kali wamejichimbia.

Wanis Bukhamada kamanda wa kikosi maalum cha Libya akitowa taarifa ya kuunga mkono kampeni ya Generali Haftar ya kutokomeza wanamgambo nchini Libya.
Wanis Bukhamada kamanda wa kikosi maalum cha Libya akitowa taarifa ya kuunga mkono kampeni ya Generali Haftar ya kutokomeza wanamgambo nchini Libya.Picha: Reuters

Vikosi vya polisi,maafisa wa kambi ya anga ya Tobruck na kabila lenye nguvu la Al Baraassa kutoka mashariki ya Libya pia wametangaza kumuunga mkobo Haftar.Hata wizara ya mambo ya ndani ya Libya imesema leo katika taarifa kwamba imeamuwa kuunga mkono kampeni ya kijeshi inayoongozwa na Generali huyo mstaafu Khalifa Haftar dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu.

Mnadhimu Mkuu wa kikosi cha ulinzi wa anga Kanali Jomaa al Abani amekiambia kituo kimoja cha televisheni ya binafsi jana usiku kuwa anajiunga na mashambulizi yanayofanywa na Haftar dhidi ya wanamgambo yaliyopewa jina "Operesheni Utu".

Wanaomkosowa Haftar wanasema amekuwa akilipwa na Marekani ambako alikuwa akiishi uhamishoni kwa miongo miwili lakini serikali ya Marekani imejitenga na generali huyo muasi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki amesema hawakuwa na mawasiliano naye hivi karibuni na hawaidhinishi au kuunga mkono mambo yanayofanyika nchini Libya hivi sasa na kwamba hawakusaidia hatua anazochukuwa.Msemaji huyo amekataa kusema iwapo Marekani inaona hatua hizo za Haftar ni jaribio la mapinduzi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman