1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa mchujo Jubilee waahirishwa Nakuru

Iddi Ssessanga
21 Aprili 2017

Hali ya sintofahamu imegubika mchakato wa kura za mchujo za chama talawa nchini Kenya, Jubilee. Katika kaunti ya Nakuru, zoezi hilo limeahirishwa baada ya wagombea kilalamikia udanganyifu na ukosefu wa mipangilio.

https://p.dw.com/p/2bhzM
Kenia Wahlen Uhuru Kenyatta und William Ruto
Wagombea wakuu wa Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William RutoPicha: Reuters

Kura za mchujo za chama tawala cha jubilee zimeahirishwa huku wagombea wakilalamikia ukosefu wa mipangilio thabiti na madai ya udanganyifu. Aliyekuwa mwenyekiti wa mamlaka ya kitaifa ya usalama barabarani Lee Kinyanjui, ambaye sasa anawania ugavana wa kaunti ya Nakuru ametaja baadhi ya visa wanavyohisi vitachangia kukosekana kwa haki katika mchakato huu.

Kasoro na madai ya udanganyifu

"Kasoro ya kwanza ni kwamba vijisanduku vya kura vilifaa vifikishwe kwenye afisi za chama hicho Nakuru kabla ya saa sita jana usiku lakini hadi tunakwenda hewani havikuwa vimefika," alisema Lee Kinyanjui.

Vingine vilifika vikiwa wazi kuonyesha kuwa makaratasi hayo yalikuwa yamechezewa. Maeneo mengi yalianza zoezi la upigaji kura kwa kuchelewa huku vituo vya molo vikikosa makaratasi ya kura ya wagombea uwakilishi wa wadi. Eneo la kuresoi lililo na zaidi ya wapiga kura elfu tatu lilipokea karatasi mia tano pekee za kura, aliongeza kusema mgombea huyo.

Kenia Unruhe Polizei
Polisi imetumia mabomu y akutoa machozi kuwatawanya waandamanaji walioanza kufanya fujo kupinga uendeshaji wa zoezi la mchujo wa chama cha Jubilee mjini Nakuru.Picha: picture alliance/dpa/D. Irungu

Wengi walisalia bila kujua nani atapiga kura na nani ataachwa nje. Hali hiyo iliyozua mtafaruku. Wapiga kura walizusha fujo katika maandamano mjini Nakuru wakilaani kile walichokiita njama ya baadhi ya wanasiasa kutumia njia ya udanganyifu kupata viti vya kisiasa. Hata hivyo, maafisa wa usalama walikuwa macho, na kuutawanya umati huo kwa kufyatua mabomu ya kutoa machozi katika juhudi za kuimarisha usalama.

Aidha, maafisa wa usalama walipinga kambi katika afisi za chama cha jubilee zilizoko Nakuru wakati vijana walipotishia kuvamia afisi hizo. Wanasiasa wametumia mamilioni ya pesa katika kinyang'anyiro cha kura za mchujo za chama cha jubilee, ikizingatiwa kuwa Nakuru ni ngome ya jubilee. Zaidi ya watu elfu 2 wamejitokeza kugombea nafasi 69 katika kura hizo za mchujo.

Nakuru huu ni uchaguzi mkuu

"Kwa Nakuru huu ni uchaguzi mkuu. Kwa hivyo kila mwanasiasa amechukua muda kupanga na kujitayarisha kwa kura hii na inatamausha kuona kuwa, licha ya usimamizi wa chama cha jubilee kuwaahidi uchaguzi dhabiti hayo hayajatimia," alisema mgombea wa kiti cha useneta Daktari Karanja Kabage.

Katibu mkuu wa chama cha jubilee tawi la Nakuru Peter Cheruyiot amethibitisha kuwa zoezi la kura za mchujo kaunti ya Nakuru limeahirishwa hadi taarifa zaidi zitakapotolewa. Rais Uhuru Kenyatta pamoja na Raphael Tuju mwenyekiti wa jopo kazi la chama cha jubilee linalosimamia shughuli za uchaguzi waliahidi zoezi litaendeshwa kwa njia shwari, huru na yenye usawa.

Mwandishi: Lexy Wakio Mbogho - DW Nakuru

Mhariri: Iddi Ssessanga