1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais nchini Urusi

Hamidou, Oumilkher29 Februari 2008

Rais anaemaliza wadhifa wake Putin awahimiza warusi wakapige kura kuhifadhi utulivu nchini.

https://p.dw.com/p/DFrX
Rais anaemaliza wadhifa wake Vladimir Putin wa UrusiPicha: AP


Rais Vladimir Putin wa Urusi amewatolea mwito wananchi wenzake wateremke vituoni kupiga kura jumapili ijayo ili "kudhamini utulivu wa Urusi" katika wakati ambapo mteule wake Dmitri MEDWEDEW anapewa kila nafasi ya kuibuka na ushindi na kuingia Kremlin tangu duru ya mwanzo ya uchaguzi itakapomalizika.


Mwishoni mwa kampeni ya uchaguzi iliyodumu mwezi mzima,rais Vladimir Putin amejitokeza katika televisheni zote za nchi hiyo leo asubuhi kuhutubia kwa mara ya mwisho kabla ya uchaguzi wa jumapili ijayo.


"Jumapili , March pili ijayo,  kuna tukio muhimu la kisiasa litakalojiri: uchaguzi wa rais wa nchi yetu.Miezi mitatu iliyopita,tumelichagua bunge jipya ambalo limeshaanza shughuli zake .Keshokutwa tutamchagua rais mpya na kwa namna hiyo tunakamilisha awamu ya pili na muhimu ya mageuzi ya uongozi nchini mwetu.Hatustahiki kusitisha mkondo wa mageuzi ya Urusi,tunabidi tuyatekeleze ipasavyo.Nnakuombeni kwa hivyo teremkeni kwa wingi vituoni mkaupigie kura mustakbal wa Urusi."


Rais  anaemaliza wadhifa wake,aliyeiongoza Urusi tangu mwaka 2000 ,na anaetazamiwa kukabidhiwa wadhifa wa waziri mkuu,amezungumzia umuhimu wa uchaguzi huo wa jumapili katika kudhamini utulivu wa nchi hiyo.

Hotuba yake imesadif saa chache kabla ya kumalizika kampeni ya uchaguzi iliyokua chapwa-hakujakua na mijadala yoyote ya kisiasa  na Dmitri Medwedew amepewa ushindi hata kabla ya uchaguzi kufanyika.


Kwa mujibu wa utafiti wa mwisho wa maoni ya umma,naibu huyo wa kwanza wa waziri mkuu na mwenyekiti wa baraza la utawala la kampuni kubwa ya gesi ya Urusi-Gasprom atajikingia kati ya asili mia 61 na asili mia 80 ya kura,akifuatiwa nafasi ya pili na mgombea wa chama cha kikoministi Guennadi Ziougganov kati ya asili mia 9-hadi 16 ya kura na mgombea anaeelemea zaidi upande wa ulaya ya magharibi Andrei Bogdanos anasemekana atajikingia kati ya asili mia 7-hadi 14 ya kura.


Mnamo wiki za hivi karibuni,Medwedew alikua kila wakati akionyeshwa katika televisheni za Urusi.Wagombea wengine watatu hawakupewa hata nusu ya muda aliokua nao mteule huyo wa rais Putin  katika televisheni za nchi hiyo.


Akihojiwa na kituo cha matangazo cha BBC,mwenyekiti wa kamisheni kuu ya uchaguzi Vladimir Tchourov amekiri kwamba wagombea  hawakuhudumiwa sawa na vyombo vya habari.Hata hivyo amemtetea Medwedev akihoji cheo chake kinamruhusu atumie muda zaidi mitamboni.


Chama cha kikoministi kimelalamika hii leo mbele ya ujumbe wa bunge la baraza la ulaya dhidi ya maandalizi ya kampeni ya uchaguzi wa rais.

Kesho,upande wa upinzani wa kiliberali ambao umeshindwa kumuandikisha mgombea wao,unapanga kuikabidhi kamisheni kuu ya uchaguzi saini za watu elfu tano mashuhuri wanaopanga kususia kile wanachokiita "kiini macho."


Eti eti zimezagaa watu wakijiuliza Vladimir Putin atafanya kazi gani baadae?Waziri mkuu wa mpito kabla ya kuustaafu,au mkuu wa serikali kabla ya kurejea tena Kremlin?






►◄