1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rais wa Umoja wa Ulaya kufanyika Mei mwaka ujao

8 Novemba 2018

Chama cha Umma wa Ulaya, EPP, leo kimemteua mbunge wa Ujerumani katika Bunge la Ulaya, Manfred Weber, kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya mwaka ujao wa 2019

https://p.dw.com/p/37u1a
Kongress der EVP in Helsinki Manfred Weber
Picha: picture-alliance/Lehtikuva/M. Ulander

Hatua hiyo imemweka Weber katika nafasi ya kugombea mojawapo ya wadhifa wakubwa katika umoja huo. Weber alipata asilimia 79 ya kura 619 zilizopigwa katika Bunge la Conservative mjini Helsinki, Finland, na kumshinda mpinzani wake aliyekuwa Waziri Mkuu wa Finland Alexander Stubb.

Chini ya mfumo wa mgombea anayeongoza, makundi ya kisiasa huwateua wanaofaa kwa nafasi ya rais wa Umoja wa Ulaya, nafasi inayoshikiliwa kwa sasa na Jean Claude Junker. Hata hivyo viongozi wa Muungano wa Ulaya lazima waidhinishe uamuzi wa mwisho. Mfumo huo ulianzishwa ili kuboresha uwazi na ushiriki wa wapiga kura katika uchaguzi wa umoja huo.

Weber, anayetoka eneo la Kusini mwa Ujerumani, Bavaria, anakiongoza Chama cha Umma wa Ulaya katika Bunge. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amempongeza na kusema amejenga daraja katika kampeni yake nyumbani kwao Bavaria na jukumu linalomsubiri katika Umoja wa Ulaya.

Kongress der EVP in Helsinki Manfred Weber Alexander Stubb
Picha: picture-alliance/Lehtikuva/M. Ulander

Mpinzani mkuu wa Weber anatarajiwa kuwa Frans Timmermans, mgombea wa Chama cha Wasoshalisti cha Ulaya. Wagombea hao wanatarajiwa kuendesha kampeni eneo zima la Ulaya kwa niaba ya makundi yao kabla ya uchaguzi wa Mei mwaka ujao, ingawa wanaweza kugombea kila mmoja katika taifa lake.

Miongoni mwa majukumu ya Rais wa Umoja wa Ulaya ni kupendekeza sheria, kuhakikisha zinaheshimiwa na kujadili mikataba na mataifa ya Magharibi, mfano biashara. Taasisi hiyo ina wafanyakazi elfu 32. Iwapo atashinda, Weber atakuwa raia wa pili wa Ujerumani kuwa Rais wa Umoja wa Ulaya, baada ya Walter Hallstein ambaye alikuwa mtu wa kwanza kushikia wadhifa huo kuanzia mwaka 1958 hadi mwaka 1967.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE/RTRE

Mhariri: Mohammed Khelef