1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Ujerumani na mvuto mdogo Afrika

10 Septemba 2013

Siasa za Ujerumani hazina mvuto mkubwa sana barani Afrika, lakini kwa wale wanaofanya kazi na Ujerumani wanammwagia sifa Kansela wa sasa Angela Merkel. Baadhi wanataka ajihusishe zaidi na bara la Afrika.

https://p.dw.com/p/19YOy
Picha: Fotolia/photocrew

Siasa za Ujerumani hazina mvuto mkubwa sana barani Afrika, lakini kwa wale wanaofanya kazi na Ujerumani wanammwagia sifa Kansela wa sasa Angela Merkel. Baadhi wanataka ajihusishe zaidi na bara la Afrika.

Timu ya waandishi wa DW ilikusanya maoni ya raia kutoka mataifa mbalimbali ya kiafrika, kuhusiana na mtazamo wao wa wagombea wa tiketi ya Kansela katika uchaguzi wa Septemba 22.

Kama ingelikuwa kwa raia wa Msumbiji waliowahi kufanya kazi katika Ujerumani ya mashariki, matokeo ya uchaguzi wa Septemba 22 yangelikuwa bayana. Kansela Angela Merkel na chama chake cha CDU na ndugu zao wa CSU wangeshinda tena.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kutoka chama cha CDU.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kutoka chama cha CDU.Picha: picture-alliance/dpa

Arnaldo Mendes, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 47 alisema kuwa, "chini ya utawala wa Merkel, Ujerumani imeendelea kuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi na imara barani Ulaya. Hata mgogoro wa kiuchumi uliyoitikisa dunia haukuwa na madhara kwa Ujerumani. Kama mimi ningelikuwa napiga kura, ningempigia kura yangu."

Sera yake ya uchumi yawavutia wengi

Katika mataifa mengine, maoni yaliyokusanywa na waandishi wa DW, yanaonyesha kuwa wananchi wanafuatilia sera ya kiuchumi ya Merkel. Jared Amba mwenye umri wa miaka 29 kutoka mji mkuu wa Kenya Nairobi, anasema Merkel amefanikiwa kuinua hadhi ya Ujerumani kimataifa ikilingaishwa na watangulizi wake, na kwamba kiongozi yeyote anaetaka kushindana naye lazima afikirie sana kiuchumi.

"Ameiweka Ujjrumani katika nafasi ya kuheshimika kimataifa ikilinganishwa na watanguzi wake kama Helmut Kohl na wengine. Ukingalia jinsi uchumi wa Ujerumani unavyoendelea, utaelewa kuwa nchi hiyo ndiyo inayasaidia mataifa yote yaliyo na uchumi unaodidimia katika Umoja wa Ulaya," alisema Amba.

Wengine kama Francis Koffi kutoka Cote d'Ivoire wanampenda Merkel kutokana na muoneko wake wa nguvu. Meite Hamed kutoka mji mkuu kiuchumi wa Abidjan, alisema jina la Merkel linahusishwa na uongozi imara na kwamba Ujerumani imeendelea kuwa taifa muhimu barani Ulaya. Lakini kwa wengine kama Jean Baptiste Kouadio, Merkel hana umuhimu kwao.

"Anawakilisha nini kwangu? Hakuna. Yeye anaiongoza Ujerumani na ndivyo hivyo," alifafanua Kouadio.

Mgombea wa nafasi ya Kansela kupitia chama cha SPD, Peer Steinbrück.
Mgombea wa nafasi ya Kansela kupitia chama cha SPD, Peer Steinbrück.Picha: Reuters

Ushiriki wa Ujerumani barani Afrika

Profesa Chacha Nyaigoti Chacha, mhadhiri wa taasisi ya maendeleo ya kanda ya Chuo Kikuu cha kikatoliki cha Afrika mashariki mjini Nairobi, anasema Kansela Merkel amejaribu kuifanya Ujerumani kuwa taifa muhimu duniani, lakini aliongeza kuwa, "sina uhakika kama amefanikiwa katika hilo, lakini kwa upande wa Afrika, sijaweza kufahamu bayana msimamo wa Ujerumani ni upi kuhusiana na Afrika."

Profesa Nyaigoti anasema Ujerumani laazima ijihusishe kwa karibu na izungumzie matatizo ya Afrika ili iweze kujulikana zaidi katika bara hilo. Lakini kwa sasa haijalishi kwa watu wengi na hata serikali, ni chama gani kinashinda uchaguzi. Profesa Nyaigoti anafafanua kuwa hakuna anayepinga kuchaguliwa tena kwa Merkel, kwa sababu siyo mtu mwenye utata na hajasababisha machafuko katika maeneo mengine ya dunia.

Peer Steinbrück safari ndefu

Kwa kulinganishwa na Merkel, mpinzani wake mkuu kutoka chama cha kisoshalisti SPD, Peer Steinbrück bado hajulikani kabisa barani Afrika.

"Peer Steinbrück? Anhaa, huyo ni mgombea wa upinzani...unajua mimi sina maslahi sana na siasa za Ujerumani, nafuatilia zaidi kile kinachoendelea nchini Msumbiji," alisema Emilia Davune kutoka Msumbiji.

Waandishi: Steffen, Sarah, Adaye, Julien, da Silva, Romeu, Kiti Alfred
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba