1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Ulaya na Chanjo dhidi ya Surua Magazetini

Oumilkheir Hamidou
6 Mei 2019

Uchaguzi wa bunge la Ulaya, mapigano kati ya wanamgambo wa itikadi kali wa Hamas katika ukanda wa Gaza na wanajeshi wa Israel na chanjo ya lazima dhidi ya maradhi ya suruwa ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/3HzKf
EU Deutschland l Pulse of Europe - Demonstration in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Tunaanza na uchaguzi wa bunge la Ulaya. Gazeti la Mittelbayerische Zeitung la mjini Regensburg linaandika: "Uchaguzi utakaoamua hatima" ndio kauli iliyoingia midomoni watu wanapozungumzia kuhusu uchaguzi wa bunge la Ulaya. Na kusema kweli uchaguzi huo utakaoitishwa Mei 26 unaashiria hali hiyo.

Wapinzani na maadui wa Umoja wa Ulaya wanaweza siku hiyo kupata sauti nyingi zaidi kuliko wakati wowote mwengine. Tokea hapo, tayari wakati huu tulio wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wanaopigania siasa kali za kizalendo wanashawishi mijadala ya kisiasa katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, naiwe kama makundi ya upinzani bungeni au sehemu ya vyama vinavyounda serikali kuanzia Hungary, kupitia Austria hadi kufikia Italia.

Katika daraja ya Umoja wa Ulaya hadi wakati huu wafuasi hao wa siasa kali walikuwa wamegawanyika makundi makundi, hawakuwa wakishirikiana. Hata hivyo, tukizingatia matokeo ya utafiti wa maoni ya wananchi, basi vyama vyote vya siasa kali za mrengo wa kulia kwa pamoja vinaweza kujikingia robo ya viti jumla vya bunge la Ulaya. Kwa hivyo, kutokwenda kupiga kura itamaanisha kuwaachia uwanja wale wanaopinga demokrasia.

Damu yaendelea kumwagika Mashariki ya Kati

 

Kwa mara nyengine tena, makombora yamefyetuliwa na jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza. Gazeti la "Rheinpfalz" linaandika: "Ndio na mara hii pia makombora yamefyetuliwa ili kujibu shambulio la wafuasi wa kundi la itikadi kali ka Kipalestina - Hamas.

Lakini Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na serikali yake ya muungano wa vyama vinavyofuata imani kali ya kidini, wakiwa madarakani kwa zaidi ya miaka kumi sasa, hawakuchukuwa uamuzi wa busara ili kuzuwia damu isizidi kumwagika. Kinyume kabisa. Wanaamini mzozo utadhibitiwa tuu. Badala ya kuisaidia ipate nguvu serikali dhaifu ya Mahmoud Abbas mjini Ramallah, badala ya kuzungumza naye, Netanyahu, akisaidiwa na Marekani, anafanya kinyume chake. Lengo lake la kuunda Israel kubwa ni la hatari. Na anahatarisha kwa namna hiyo pia maisha ya raia wake mwenyewe."

Chanja dhidi ya surua iwe ya lazima

 

Waziri wa Afya wa serikali kuu ya Ujerumani, Jens Spahn, anapanga kulazimisha watoto wa shule za chekechea wachanjwe dhidi ya maradhi ya surua, la sivyo hatua kali zitachukuliwa. Gazeti la Hannoversche Allgemeine linazungumzia kuhusu uamuzi huo. Bila ya shaka Spahn anafanya kile kinachostahiki kufanywa.

Lakini kwa bahati mbaya anafikia nusu njia. Kwa sababu takwimu zinaonyesha katika kadhia za hivi karibuni za maradhi ya surua, takribani nusu ya walioshikwa na maradhi hayo ni watu wazima. Na hasa katika hirimu hiyo ndio kuna uhaba wa watu waliochanjwa dhidi ya surua.

Kwa hivyo, haitoshi Spahn anaposhinikiza katika shule za chekechea walimu na wasimamizi lazima wachanje. Ni sawa kulazimisha chanjo kwa watu wazima haitakuwa rahisi, kama ilivyo kwa watoto. Hata hivyo, lingekuwa sharti muhimu ili kupiga vita surua na maradhi mengine ya hatari yanayoambukiza.

 

Mwandishi: Hamidou Oumilkhheir

Mhariri: Mohammed Khelef