1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Urusi magazetini

Hamidou, Oumilkher3 Machi 2008

Kuchaguliwa Medwedew kushika nafasi ya Putin na mvutano ndani ya chama cha SPD

https://p.dw.com/p/DH0p
Medwedew na Putin ´baada ya uchaguziPicha: AP



Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamejishughulisha zaidi na uchaguzi wa rais nchini Urusi na mvutano unaoendelea ndani ya chama cha Social Democratic cha Ujerumani-SPD,kama washirikiane na chama cha mrengo wa shoto Die Linke au la.


Kuhusu uchaguzi wa Urusi ,gazeti la HANDELSBLATT linaandika:


"Opereshini,nani awe mrithi" imekamilishwa:baada ya uchaguzi wa jana,mbabe wa Urusi Vladimir Putin anaweza kushusha pumzi,mbinu za kuchaguliwa DMITRI MEDWEDEW kua rais wa Urusi zimefanikiwa.Kitakachofuatia hivi sasa hakijawahi hata mara moja kushuhudiwa katika historia ya Urusi.Kiongozi mwenye nguvu kupita wote wa nchi hiyo,mwenye kujiamini na mwenye shauku,anang'atuka na badala yake anakubali kukabidhiwa wadhifa mdogo wa waziri mkuu."


Hayo ni maoni ya HANDELSBLATT.DIE LADENSZEITUNG la mjini Lüneburg linasema uchaguzi haukua wa kidemokrasi.Gazeti linaendelea kuandika:


"Baada ya vituo vya upigaji kura kufungwa,Kremlin ilisubiri saa moja tuu  kabla ya kumtangaza DIMITRI MEDWEDEW kua mshindi.Lakini MEDWEDEW hawezi kudai amechaguliwa kwa njia halali.Anaandamwa na dosari sio tuu ya kua kibaraka cha Putin,bali pia dosari kwamba uchaguzi ulikua wa udanganyifu.Putin amevikaba vyombo huru vya habari,wagombea wa kiliberali hawajaruhusiwa na wapiga kura milioni 110 wamelazimishwa wateremke kwa kila hali vituoni kumpigia kura yule aliyetajwa kua  "mwenye kustahiki".


 Hata kama uchaguzi ungekua wa kidemokrasi Medwedew pengine angeshinda" linahisi gazeti la RHEINISCHE POST la mjini DÜSSELDORF.


"Kwanza kwasababu upande wa upinzani haukua na mpango wowote wa kuridhisha kuweza kushindana na mfumo wa Putin.Na pili,wananchi wengi wa Urusi wanaamini wanaweza hivi sasa kujivunia hali ya utulivu na neema nchini mwao,kutokana na utawala wa Putin na kundi lake.


FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND linamchambuaa mshindi wa ushaguzi wa Urusi na kuandika:


Kwa vyovyote vile DIMITRI MEDWEDEW ana tabia inayowapa watu matumaini mema.Yeye kinyume na  wakuu wa Kremlin hatokani na idara ya upelelezi inayoangaliwa kama chombo cha kukandamiza watu nchini Urusi.Hafuati sera za uchumi wa mpangilio na wala hayumo katika kundi la wenye kutoa maneno makali dhidi ya Ulaya na Marekani."


Mada ya pili magazetini inaturejesha humu humu nchini Ujerumani.Mvutano ndani ya chama cha Social Democratic-SPD kama washirikiane au la na chama cha mrengo wa shoto Die Linke,ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG.


Mashaka gani haya yaliyosababishwa na Kurt Beck?Kwanza anavunja ahadi na kuchochea mageuzi ya fikra kuhusu chama cha mrengo wa shoto Die Linke.Baadae baadhi ya viongozi wa SPD wakaonyesha kuridhia kabla ya wengine kuanza kupaza sauti kupinga msimamo wake.Na sasa kuna wanaofika hadi ya kushuku kama anapaswa kugombea wadhifa wa kansela.Mzozo usiokwisha ndani ya SPD umechukua sura ya  mvutano wa kuania uongozi ndani ya chama hicho.


Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linakosoa kigeu geu cha BECK.Gazeti linaendelea kuandika:


Kigeu geu cha SPD jimboni Hessen ni kinyume na ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi jimboni humo.Bila ya kujali nini kiko nyuma ya mbinu hizo,kigeu geu hicho kinachafua uaminifu wa SPD.Hakuna atakaeamini  eti SPD watashirikiana na Die Linke katika daraja ya kijimbo tuu ,lakini katika daraja ya shirikisho,ni muhali.