1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Uturuki na Mzozo wa wakimbizi Magazetini

Oumilkheir Hamidou
25 Juni 2018

Uchaguzi mkuu nchini Uturuki, uhusiano kati ya Marekani ya Donald Trump na washirika wake wa magharibi na mzozo wa wakimbizi ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/30DZf
Türkei Wahl Tageszeitung
Picha: Getty Images/AFP/O. Kose

Tunaanzia Uturuki ambako uchaguzi mkuu ulioitishwa jana umempatia ushindi rais RecepTayyip Erdogan na chama chake cha Kiislam  AKP. "Si ushindi mkubwa hivyo" linaandika gazeti la kusini magharibi mwa Ujerumani "Stuttgarter zeitung". Gazeti linaendelea kuandika: "Hata kama siku  za mbele Erdogan atakuwa takriban akiongoza peke yake kwa kutia saini kanuni, pigo la kupoteza wingi mkubwa wa kura chama chake cha AKP ni kubwa mno kuweza kupuuzwa.

Matokeo ya uchaguzi yanabainisha kwa mara nyengine tena: Uturuki imegawika sana. Erdogan angefanya la maana kuondowa mfarakano. Na hilo lingekuwa na faida pia kwa uchumi. Uchumi utakabiliwa na hali ngumu ikiwa rais hatofanikiwa kurejesha imani ya wananchi na wawekezaji.Tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kama rais mwaka 2014 Erdogan aliahidi "atakuwa rais wa waturuki wote". Ahadi hiyo lakini mpaka leo haijatekelezwa.

Uhusiano kati ya Marekani na washirika wa magharibi

Mada ya pili magazetini inamulika uhusiano kati ya Marekani na washirika wake wa magharibi. Gazeti la kaskazini mwa Ujerumani "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Hofu imeenea ikulu ya Marekani-White House. Miezi takriban mitano kutoka sasa wamarekani watalichagua bunge jipya la Congress. Na mpaka sasa hakuna anaeweza kuashiria kama wa-Republican watafanikiwa kutetea wingi wa viti vyao katika mabaraza yote mawili ya bunge hilo.

Kutokana na hali hiyo ya kutokuwa na uhakika, Donald Trump anategea mkakati ambao umeshampatia maarifa makubwa maishani mwake: Anapalilia mambo na kuzidisha makali mivutano ili kuwahamasisha wafuasi wake. Na Ujerumani inakamata nafasi muhimu katika karata hizo. Mtu anaweza kufikiri kuwa hiki ni kiroja kwamba washirika wakubwa wa siasa ya nje ndio rais wa Marekani anaowaangalia kuwa wakinzani wa kuandamwa kwa kila hali.

Kama anavyowaandama wapinzani wake wa ndani kutoka chama cha Democratic, ndivyo Trump anavyoiangalia Berlin. Kiongozi wa upinzani katika bunge la Marekani hukaripiwa takriban sawa sawa na inavyokaripiwa serikali kuu ya Ujerumani. Katika wakati ambapo washirika wa nchi zinazopakana na bahari ya Atlantik wanaikumbuka miaka 70 ya misaada iliyokuwa ikidondoshwa angani badala ya mabomu ,vita vikuu vya pili vya dunia vilipomalizika,Trump yeye ana mengine kichwani; na hayahusiani kabisa na kudondosha zabibu kutoka anga ya Berlin.

Merkel na shinikizo la wakimbizi

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na mzozo wa wakimbizi na kishindo anachokabiliana nacho kansela Angela Merkel. Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linazungumzia mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi na kuandika:"Angela Merkel anajaribu kwa kila hali kuunusuru wadhifa wake serikalini. Enzi za kusubiri ufumbuzi wa pamoja wa Umoja wa Ulaya kuhusu wakimbizi zimekwisha-CSU wamezikomesha.

Merkel atalazimika kupata ufanisi mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakapoitishwa Alhamisi inayokuja-dhamiri njema pekee hazitoshi.Ufanisi kama huo unaweza kutuwama katika suala la kuimarishwa ulinzi wa mpakani unaostahiki jina hilo. Mkutano wa maandaalizi ulioitishwa Jumapili unaashiria la maana. Ujerumani inaweza kuchangia wanejeshi na polisi pia katika kikosi kipya cha ulinzi wa mipaka.

 

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga