1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Zimbabwe huendausiwe wa huru na haki

Mwakideu, Alex19 Machi 2008

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti inayotilia shauku kufanyika kwa uchaguzi wa haki na huru nchini Zimbabwe

https://p.dw.com/p/DRJP
Rais Robert Mugabe ahutubia wafuasi wa chama cha ZANU PFPicha: picture-alliance/ dpa

Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 mwezi huu nchini Zimbabwe huenda usiwe wa huru na haki. Hayo ni kulingana na Shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch.


Shirika hilo limetaja hujuma dhidi ya wanasiasa wa upinzani, vikwazo dhidi ya mikutano ya hadhara na kuwanyima wanahabari haki ya kutekeleza wajibu wao nchini Zimbabwe kama baadhi ya sababu zinazoashiria kwamba uchaguzi huo hautakuwa wa haki.


Hivi maajuzi serikali ya Zimbabwe kupitia Rais wake Robert Mugabe imewagawia wananchi vyakula na vifaa vya ukulima; jambo ambalo shirika la kutetea haki za kibinaadamu la Human Rights Watch linasema ni utumizi mbaya wa fedha za serikali katika kampeni za Rais wa nchi hiyo.


Rais Mugabe mwenye miaka 84 anatarajiwa kushinda uchaguzi wa Urais.


Wapinzani wake wa karibu ni Morgan Tsyangirai kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change na aliyekuwa waziri wa fedha na pia kiongozi wa zamani wa chama cha ZANU PF Simba Makoni.


Wafuasi wa Rais Mugabe wamekuwa wakitumia ghasia kuwahujumu wale wa upinzani kabla ya uchaguzi wa wiki ijayo na shirika la Human Rights Watch limesema jambo hilo litafanya uchaguzi huo usiwe wa haki.


Mugabe anakabiliwa na changamoto kali zaidi katika miaka yake 28 ya utawala kutokana na kuzorota kwa uchumi wa nchi hiyo pamoja na hatua ya baadhi ya viongozi wa chama tawala cha ZANU PF ya kujiondoa chamani.


Sawa na chaguzi zilizopita viongozi wa mabaraza ya miji, wafuasi wa chama cha ZANU PF na walinda usalama wakiwemo polisi na wapelelezi wametajwa katika ripoti hiyo iliyotolewa mjini Johannesburg Afrika Kusini kama wakiukaji wakubwa zaidi wa sheria za uchaguzi.


Wapinzani wamelalama kwamba Mugabe amekuwa akishinda chaguzi nchini Zimbabwe kupitia udanganyifu; jambo ambalo Rais huyo anapinga vikali.


Kiongozi wa Human Rights Watch barani Afrika Georgette Gagnon amesema licha ya maendeleao kuhusu sheria za uchaguzi yaliyofanywa katika makaratasi raia wa Zimbabwe bado hawajakuwa huru kumchagua mgombea wanaompenda zaidi.


Wakati wagombea 4 wamejitokeza kung'ang'ania kiti cha Urais, na vyama kadhaa vimejitokeza kushiriki katika uchaguzi wa mwezi huu, njia ambazo zinatumika katika uchaguzi wenyewe zina itilafu. Limesema shirika la Human Rights Watch.


Matamko ya viongozi wawili wa usalama kwamba hawatakubali vyama vya upinzani vishinde katika uchaguzi wa mwezi huu yamezua hali ya sitofahamu katika kampeni za uchaguzi huo ambazo hadi sasa zimeendelea kwa amani.


Wananchi wa Zimbabwe wanateseka kutokana na mfumuko wa bei wa hali ya juu zaidi kote duniani unaozidi asilimia 100,000 pamoja na uhaba wa vyakula, mafuta na ukosefu wa pesa za kimataifa.


Shirika la Human Rights Watch limesema limeitoa ripoti yake baada ya uchunguzi wa wiki 7 uliyofanywa katika mikoa 10 nchini Zimbabwe.


Bei za bidhaa za kawaida kama unga wa mahindi, mkate, mafuta ya kupikia na sabuni zimepanda kwa asilimia 300 tangu mwanzoni mwa mwezi huu.


Rais Mugabe amekuwa akilaumu Uingereza na Marekani kwa kuzorota kwa uchumi wa nchi hiyo.


Ametishia kufanya msako mkali kwa viongozi wa biashara wanaopandisha bei za bidhaa akisema kwamba hiyo ni njama ya kuwafanya wapiga kura wasiichague serikali yake.


Baadhi ya wafanyibiashara wamekamatwa na kwa kile ambacho serikali ya Zimbabwe inasema ni kuongeza bei za bidhaa bila idhini yake.


Rais Mugabe ametawala Zimbabwe tangu nchi hiyo iliponyakua uhuru kutoka mikononi mwa Uingereza mwaka wa 1980.