1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi waahirishwa Pakistan

2 Januari 2008

Rais Musharraff akihutubia taifa,Tume ya uchaguzi imeahirisha uchaguzi hadi Februari 18.

https://p.dw.com/p/CjQq

Uchaguzi mkuu nchini Pakistan kama iliovyotazamiwa umeahirishwa hii leo kwa muda wa wiki 6-yaani hadi kati ya mwezi ujao-Februari 18.Hii inatokana na machafuko yaliofuatia kuuwawa kwa aliekua waziri-mkuu bibi Benazir Bhutto .Vyama 2 vikuu vya upinzani nchini Pakistan pamoja na kile cha marehemu Pakistan Peoples’Party, vimepinga uamuzi huo.Chama cha pili kikuu cha upinzani cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Shariff kimetangaza sasa kwamba kitashiriki katika uchaguzi huo ulioahirishwa.Rais Musharraff anatazamiwa hivi punde kulihutubia Taifa:

„Katika mikoa yote 4 ,utaratibu wa kuendesha uchaguzi ulisimama kwa siku kadhaa.“alisema mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Qazi Mohammad Farooq, alienadi kwamba uchaguzi sasa utafanyika Februari 18 badala ya januari 8.

Farooq alisema afisi 11 katika wilaya ya sindh,anakotoka marehemu Benazir Bhutto,zilichomwa moto wakati wa machafuko na kuteketeza masanduku ya kutilia kura ,orodha za wapigakura na zana nyengine za uchaguzi.

Wafuasi wa chama cha upinzani cha Pakistan People’s Party cha Benazir bhutto na kile cha Muslim League cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif,wakitaka uchaguzi ufanyike kama ilivyopangwa vikihofia kuuchelewesha kungemnufaisha rais Pervez Musharraff.

„Sababu zozote walizotoa ni kisingizio tu kwa sababu orodha za wapigakura ndio zilichomwa moto wilayani lakini wanazo orodha hizo katika afisi kuu.“ alisema Farzna Raja,msemaji wa chama cha bibi bhutto cha Pakistan Peoples’ Party:

Chama cha Bibi Bhutto kikitarajia kunufaika na uchaguzi wa mapema kutokana na huruma za wapigakura kwa kuuwawa kwa kiongozi wake wakati akiondoka kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni ya uchaguzi huko Rawalpindi.

Kiasi cha watu 60 waliuwawa katika hujuma iliofuatia ghasia zilizozuka.

Punde hivi,rais Pervez Musharraff anatazamiwa kulihutubia taifa .Mshirika wake wa chanda na pete amefichua kwamba, Musharraff atarangaza anaomba msaada wa kimataifa kuchunguza mauaji ya bibi Bhutto.

Kizuka wa marehemu bibi Bhutto, Asif Ali Zardari,mwenyekiti mpya wa chama cha PPP pamoja na mwanawe wa miaka 19 Bilawal,wameitisha kikao cha chama vaadae hii leo.

Chama kingine cha upinzani cha waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharif-Muslim League, kimedai kwamba vyama vya upinzani viungane na kuwa na msimammo mmoja kudai kujiuzulu kwa rais Pervez Musharraff pamoja na Tume ya Uchaguzi.

Msemaji wake akasema na ninamnukulu,

„Jamadari musharraff ameshindwa kuweka usalama nchini na tume ya Uchaguzi imeshindwa kufanya uchaguzi kwa wakati uliopangwa.“

Marehemu Benazir Bhutto akionekana kwa daraja ya kimagharibi akichukua msimamo wastani na alikuwa mpinzani mkali wa itikadi kali za kiislamu.Alirejea Pakistan kutoka uhamishoni hapo Oktoba na mara tu kuwasili kwake nyumbani alikosewa chupuchupu kuuliwa katika jaribio lililochukua maisha ya watu wengine 140.

Kifo cha Benazir Bhutto kilivuruga mipango na matumaini ya Marekani ya kugawana madaraka kati ya Musharraf na Benazir Bhutto .Jamadari Musharraff alinyakua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi yasio-mwaya damu .