1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin8 Machi 2007

Miongoni mwa mada zilizogonga vichwa vya habari katika magazeti ya Ujerumani leo hii ni matamshi ya baadhi ya maaskofu wa Kikatoliki,wakati wa ziara yao nchini Israel,ambayo ilitazamwa kama ni hatua nyingine ya upatanishi.

https://p.dw.com/p/CHTX

Gazeti la TAGESZEITUNG kutoka Berlin likieleza maoni yake kuhusu matamshi yaliyolinganisha hali mbaya iliyopo katika maeneo ya Kipalestina na maangamizi makuu ya Wayahudi linasema:

„Ni mwiko hasa kwa Wajerumani,kuilinganisha kwa njia yo yote ile Israel ya hii leo,na maafa yaliotokea wakati wa utawala wa Nazi.Kwa hivyo ni wazi kabisa kwamba maaskofu wamekosea walipotumia maneno hayo.Hata hivyo lakini,hamaki za mara kwa mara za balozi wa Israeli,zinataka kuvutia mawazo kwengine kabisa na kutoonyesha kuwa asingependa kusikia ukosoaji wo wote wa nchi yake.Lakini kundi lililokwenda kutembea Israel,lingesema nini kuhusu ule ukuta mkubwa ambao kwa njia fulani unautenga mji wa Bethlehem?

Wakati huo huo gazeti la WIESBADENER KURIER linakosoa kwamba:

„Hii si mara ya kwanza kwa wawakilishi wa jumuiya ya Wayahudi wa Kijerumani,bila ya kufikiria zaidi,kutamka kwamba ni “chuki dhidi ya Uyahudi“.Kitendo kama hicho hakiwasaidii wao wala jamii ya Kijerumani.Kutumiwa kwa maneno hayo mara kwa mara,hupunguza uzito wa vile vitendo halisi vya kuchukia Uyahudi. „

Kwa upande mwingine gazeti la KIELER NACHRICHTEN limechukua msimamo mkali kuhusika na matamshi ya maaskofu.Linaeleza hivi:

„Tarifa rasmi ya Baraza la Maaskofu wa Kikatoliki pamoja na shauku kubwa ya kujaribu kueleza yale yaliyotamkwa,huonyesha kuwa wakuu hao wa kanisa walijiropokea bila ya kufikiri.Hata hivyo,hilo halibadili hali kuwa bora.Kwani waliyozongwa kwa yale walioshuhudia wakati wa ziara yao,ni wajumbe muhimu wa makanisa ya Kikatoliki ya Ujerumani na sio wanafunzi wasiofahamu cho chote.“

Sasa tutupie jicho mada nyingine.Kufuatia mgogoro wa uongozi wa juma moja,sasa yadhihirika kuwa chama cha kisoshalisti cha Ujerumani SPD,katika jimbo la Hamburg kipo tayari kufungua ukurasa mpya.Chama hicho kimemteua waziri wa zamani wa utamaduni Michael Naumann kuwa mgombeaji wake mkuu katika uchaguzi wa mwaka 2008.

Gazeti la GENERAL-ANZEIGER likitoa maoni yake kuhusu uteuzi huo linasema:

„Hivyo ndio ngome ya zamani inavyoteketezwa.Baada ya msako mkubwa na shinikizo la wakuu wa chama, sasa Michael Naumann,kama mgombea uchaguzi, atakumbana na meya Ole von Beust wa chama cha CDU anaependwa na umma.Inashangaza kuwa yeye ndie aliyechaguliwa,lakini Naumann si mgeni katika jimbo la Hamburg.Kwani yeye ni mmojawapo wa wachapishaji wa gazeti maarufu la Die Zeit linalochapishwa kila juma mjini Hamburg.Sasa basi ndio ana kazi ya kukichangamsha chama cha SPD. Mshabiki huyo wa utamaduni,huenda akatoa changamoto kali kwa Ole von Beust,lamalizia gazeti la GENERAL ANZEIGER.