1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin11 Desemba 2006

Magazeti ya Ujerumani leo hasa yamejishughulisha na uchunguzi unaofanywa kuhusu kifo cha wakala wa zamani wa Kirussi,Alexander Litvinenko ambacho yasemekana kuwa kilisababishwa na sumu.

https://p.dw.com/p/CHUF

Gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG linasema

“Sasa mwendesha mashtaka wa serikali mjini Hamburg,anasadiki kuwa wakala wa zamani wa Kirussi Dmitri Kovtun si muhanga tu bali huenda ikawa ni mkosefu vile vile na uchunguzi unafanywa dhidi ya mfanya biashara huyo wa Kirussi. Inadhaniwa kuwa Kovtun huenda ikawa alileta Polonium 210 nchini Ujerumani kutoka Ururssi na baadae akaipeleka Uingereza na hivyo ameacha alama dhahiri za sumu hiyo.Lakini kwa nini njia hiyo ilitumiwa kumuua Litvinenko.Je,Kovtun ataweza kuwa katika hali ya kutoa maelezo zaidi?

Kwa maoni ya gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG mjini Düsseldorf:

“Jawabu la suala linalohusika na kifo cha Litvinenko lipo huko Moscow.Uchunguzi wa kifo chake unaongozwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai ya Uingereza yaani Scotland Yard kwa sababu mauaji hayo yametokea katika ardhi ya Uingereza. Litakuwa jambo la busara kama maafisa wa Kirussi watasaidia kwa vitendo,kupata majibu kwa masuala yaliyozuka.Kwani ni muhimu pia kwa maslahi ya Urussi kuona ukweli ukifichuliwa.”

Na gazeti la BERLINER ZEITUNG linasema:
”Licha ya kutolewa maelezo ya kutokuwa na hatia, mkasa wa Litvinenko utaathiri uhusiano wa Urussi pamoja na Uingereza na Umoja wa Ulaya kwa jumla.Kwa sababu ya maelezo yanayopingana,nchi za magharibi zinahisi kuwa Urussi si mshirika anaeweza kuaminiwa na Urussi kwa upande wake inaamini nchi hizo hazina nia njema.Na linapozuka suala la kushiriki katika mkakati muhimu,shaka huwa kubwa zaidi kuliko juhudi za kupata faida za kikazi.”

Sasa hebu tutupie jicho mada nyingine iliyoshughulikiwa na magazeti ya Kijerumani. Pendekezo la kuanzisha malipo ya ushuru wa barabara kwa magari ya binafsi,limezusha mabishano ya kisiasa nchini humu.Chama cha CSU kinatazama ikiwa serikali ipo tayari kuchukua hatua hiyo kwa kuungwa mkono na vyama vya CDU na SPD.Gazeti la OSTSEE-ZEITUNG kutoka Rostock likieleza maoni yake linasema:

“Kila wakati,suala hilo linazidi kujadiliwa kwa makini na inavyoonyesha,kuna uwezekano mkubwa kuwa waendesha magari wa Kijerumani ambao tangu hapo hawana pesa hivyo,sasa mara nyingine tena serikali itawapokonya pesa.Eti mizigo inayosababishwa kwa kushusha ushuru wa mafuta, mazingira au kodi inayolipwa na malori kwa matumizi ya barabara kuu,inahitaji kusawazishwa-ahadi kama hizo,mtu anaruhusiwa kabisa kuwa na shaka nazo lamalizia Ostsee Zeitung.