1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin27 Novemba 2006

Mkutano wa chama cha CDU mjini Dresden ni mada kuu iliyoshughulikiwa na magazeti mengi ya Ujerumani leo hii.

https://p.dw.com/p/CHUM

Wakati huo huo waziri mkuu wa North-Rhein Westphalia,Jürgen Rüttgers anajikuta kati kati ya mgogoro uliozuka ndani ya chama hicho cha kihafidhina kuhusu mwelekeo wa chama.

Kwa maoni ya gazeti la STRAUBINGER TAGBLATT, mkutano wa Leipzig uliohusika na mageuzi ni sehemu ya historia ya chama cha CDU - ni mripuko wa ushujaa wa muda mfupi tu.Likiendelea linasema Angela Merkel wakati huo akiwa kiongozi wa upinzani alidhihirika kwa ushupavu kama mwana mageuzi na sasa kama Kansela ameweza kuchukua jukumu la kurekebisha na kupatanisha.

Kwa upande mwingine MITTELBAYERISCHE ZEITUNG kutoka Regensburg linasema,Kansela Merkel ana mikakati miwili.

Likiendelea kufafanua linasema: ”Rüttgers atakumbatiwa - na pendekezo lake la kutaka malipo ya ukosefu wa ajira kurefushwa litaidhinishwa, licha ya kuwepo manungúniko ya wanauchumi katika chama cha CDU.Wakati huo huo lakini Kansela Merkel atawazingatia marafiki wanaotoa ajira na wanaotaka kuona mageuzi makali.Hata pendekezo lililotolewa na waziri mkuu wa mkoa wa Baden-Württemberg,Günther Oettinger kuwa kinga za kuachishwa kazi ziregezwe,huenda likaidhinishwa pia kwenye mkutano wa CDU mjini Dresden.

Tukiendelea na mada hiyo hiyo,gazeti la FRÄNKISCHE TAG kutoka Bamberg linasema:

“Merkel ataibuka kwa usalama kwenye mkutano huo kwani atawazimua mahasimu wake.Hapo mtu hawezi kuzungumzia msingi imara wa mamlaka linasema Fränkische Tag.Mambo yataendelea kama kawaida na siasa zinazopoteza wakati na nguvu huku Merkel mara kwa mara akilazimika kwenda nazo.

Sasa hebu tutupie jicho mada nyingine.

Vyama vya SPD na CDU vinazidi kushinikiza kuwa waajiriwa wanufaike zaidi kutokana na faida za mashirika wanayofanyia kazi.Kwa hivyo,siku ya jumanne chama cha CDU katika mkutano wake mjini Dresden kinataka kupitisha uamuzi wake kuhusu suala hilo.

Kuhusu mada hiyo gazeti la mjini Berlin TAGESZEITUNG linasema:

Cha kushangaza ni kwamba hata wakigawana faida,waajiriwa hawatonufaika.Sababu ni kwamba iwapo kutaanzishwa mfumo wa kuambatanisha mshahara na uwekezaji,basi makampuni yataweza kuweka kanuni ambazo huenda zikawafanya waajiriwa kuwa washirika.Ni dhahiri kuwa mkataba utasema:badala ya mshahara,wagawane faida.Kwa waajiriwa,huo ni mchezo wa hatari kwani daima watakuwa wakiishi katika hali hatari ya kuwepo uwezekano wa kupatikana faida ndogo zaidi kuliko vile ilivyotabiriwa,linamalizia Tageszeitung kutoka Berlin.