1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

P.Martin8 Novemba 2006

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Jumatano hasa wamejishughulisha na mgogoro unaohusika na Uturuki kuingia katika Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHUW

Mada nyingine iliyoshughulikiwa ni mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG linasema “Jamii ya Waturuki inazidi kuvunjika moyo kuhusika na Ulaya.Waislamu wamevunjika moyo kwa sababu katika mgogoro unaohusika na vazi la hijabu,walitaraji kuona Umoja wa Ulaya ukishinikizwa zaidi na viongozi wa kijeshi wasioegemea katika dini. Wakati huo huo wanajeshi wenye fikra za kizalendo wamechukizwa na usafihi wa Wazungu kuingilia mambo ya ndani ya Uturuki-hapo linalozingatiwa ni suala la Cyprus.

PFORZHEIMER ZEITUNG likiendelea na mada hiyo linasema:

Ni haki kuipa Uturuki nafasi ya kuonyesha uwezo wake kwamba inafaa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya au la.Jambo moja limeshadhihirika:Kinyume na fikra za wengi waliokuwa na shaka,majadiliano ya uanachama haimaanishi kuingia moja kwa moja katika Umoja wa Ulaya.Yule anaetekeleza masharti yote ndio anaruhusiwa kujiunga na umoja huo.Hicho ndio kinachotakiwa;labda jambo hilo ni gumu kwa Uturuki lamalizia Pforzheimer Zeitung.

Sasa tunatupia jicho mada nyingine-yaani mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

ALLGEMEINE ZEITUNG kutoka Mainz linasema:

“Mkutano unaoendelea hivi sasa mjini Nairobi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani usingeweza kufanywa mahala bora zaidi:kwani kusini mwa mji huo,pasipo kuwepo mawingu,watu wanaweza kuuona mlima wa Kilimanjaro wenye urefu wa kama mita 6,000.Kwa miaka na miaka vilele vya Kibo na Mawenzi viligubikwa kwa barafu,lakini hii leo ni mabakio madogo tu ya barafu yanayoonekana:na walinzi wa mazingira wanajitahidi kuzuia hasara zaidi.Sasa hata nchini Marekani kuna matumaini ya kuwepo mtazamo mwingine kuhusu mazingira,baada ya Arnold Schwazenegger binafsi kama gavana wa California kuitumia kisiasa mada hiyo.”

HEILBRONNER STIMME nalo linasema

Sasa hata wale wanasiasa ambao hapo zamani hawakuweza kuelezwa kama watetezi wa mazingira,wanaonya juu ya athari za kuongezeka ujoto duniani.Mmoja wao ni waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair.Vile vile Umoja wa Ulaya utakaoongozwa na Ujerumani hivi karibuni itakaposhika wadhifa wa urais,umepanga kushughulikia zaidi suala la mazingira.Kinyume na ilivyokuwa hizo siku za nyuma ulinzi wa mazingira si suala linaloshughulikiwa na wanaharakati wa mazingira tu.Ulinzi wa mazingira sasa limekuwa suala la kisiasa na litazidi kuchukua nafasi kubwa katika sekta ya uchumi lamalizia Heilbronner Stimme.