1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi, ardhi na wakimbizi vyatawala madahalo wa pili Kenya

Admin.WagnerD4 Machi 2013

Mdahalo wa mwisho wa urais nchini Kenya umefanyika, ukiwashirikisha wagombea wote wanane wa nafasi hiyo ya juu kabisaa, huku uchumi, ardhi na wakimbizi vikichukua nafasi kubwa.

https://p.dw.com/p/17lkV
The eight Kenyan presidential aspirants Mohammed Dida, James Ole Kiyiapi, Uhuru Kenyatta, Peter Kenneth, Musalia Mudavadi, Martha Karua, Kenyan Prime Minister Raila Odinga and Paul Muite (L-R) face off in the first ever presidential debate at Brookhouse School in Kenya's capital Nairobi February 11, 2013. The presidential television debate - the first ever held in the country - failed to produce a clear winner, but gave an early taste of what is expected to be a highly charged contest to run East Africa's economic powerhouse. Picture taken February 11, 2013. REUTERS/Stringer (KENYA - Tags: ELECTIONS POLITICS)
Kenia Präsidentschaftswahl Kandidaten DebattePicha: Reuters

Mdahalo huo uliyorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio ulianza kwa swala la uchumi na jinsi kiongozi atakayechaguliwa atakavyoshughulikia swala la matumizi ya fedha. Akijibu swali hilo, waziri mkuu Raila Odinga anayegombea kupitia chama cha ODM na Muungano wa Cord alisema: “Kwa wakati huu matumizi ya serikali yako juu sana na tutapendekeza kupunguzwa kwa viwango vya mishahara kuanzia na mimi mwenyewe mshahara wangu wa urais ili niongoze kwa mfano.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wakihakiki vifaa vya kupigia kura mjini Nairobi Februari 13, 2013.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wakihakiki vifaa vya kupigia kura mjini Nairobi Februari 13, 2013.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Umiliki wa ardhi, Kenyatta abanwa

Tatizo la umiliki wa ardhi ambalo limekuwepo tangu Kenya ijinyakulie Uhuru kutoka kwa Waingereza likafuatia. “Baada ya Uhuru swala hilo halikushughulikiwa hata kidogo isitoshe watu wa Pwani ndio walionyanyaswa zaidi na serikali tatu zilizopita. Kwa sababu hata hati za kumiliki ardhi zilipewa watu kutoka bara na sio wale ambao asili yao ni huko Pwani,” alisema Paul Muite Mgombea Kiti cha Urais kwa tikiti ya chama cha Safina.

Swala hilo la umiliki wa ardhi lilijadiliwa kwa kina kwenye mdahalo huo huku baadhi ya wagombea wakimpaka tope mpinzani wao Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta wakidai kwamba hataweza kushughulikia swala hilo kikamilifu akichaguliwa rais kutoakana na yeye mwenye kuwa moja wa wamiliki wa maeneo makubwa ya ardhi.

"Kwa mfano rafiki yangu Uhuru Kenyatta familia yake ni moja ya watu wanaomiliki kiasi kikuba cha ardhi nchini Kenya na tutakapoanza kuwapa makao watu wasio ardhi tutalenga ardhi isiyotumika na kwa ajili hiyo ninaamini kwamba mtu kama huyo hafai kutekeleza yale wananchi wanayotaka," alisema Martha Karua, mgombea mwanamke pekee wa kito hicho cha urais.

Akijitetea dhidi ya tuhuma hizo, mgombea Uhuru Kenyatta  alisema yeye na familia yake hawakupata ardhi mahali popote kinyume na sheri isipokuwa kwa kununua kutoka kwa wauzaji wa hiari na kwamba wametumia ardhi hiyo kwa uzalishaji kuimarisha uchumi.

Duwa ya kila moja ni kuepuka matukio kama hili la mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya 1,200 walipoteza maisha na maelfu wengine kupoteza makaazi yao.
Duwa ya kila moja ni kuepuka matukio kama hili la mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya 1,200 walipoteza maisha na maelfu wengine kupoteza makaazi yao.Picha: AFP/Getty Images

Kigugumizi kuhusu wakimbizi

Hadi sasa kuna wakimbizi wa ndani kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambao hawajapewa makao. Wagombea hao walipata wakati mgumu kueleza vipi watakavyotatua shida hiyo ambayo hasa ilitokana na tatizo la ardhi.

"Ningependa sana kuona kwamba hatuna wakimbizi wakindani kwa sababu ya siasa. Shida ambayo ilitokea ni kwamba pesa ambazo zilikuwa zimetengwa kuna wale ambao wana mashamba makubwa na wanajulikana wengine, wao wanaenda kupeana mashamba yao yanunuliwe alafu wanajaribu kuweka mnada wa bei ghali alafu serikali inashindwa kuyanunua,” alisema mgombea wa muungano wa Amani, Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi.

Mdahalo huo ambao umefanyika wiki moja kamili kabla kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kihistoria umezidi kuwafungua macho wapiga kura. Wengine hata hivyo wanasema mdahalo huo hautabadili msimamo wao. Mambo yote yaliyojadiliwa yametokana na maswali yaliyowasilishwa kwa waandalizi wa mdahalo huo baada ya mdahalo wa kwanza uliofanyika wiki mbili zilizopita. Kila mgombea amepata nafasi sawa ya kuuza sera zake. Huku kila mmoja akijinaki kuwa bora kuliko wengine.

Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Josephat Charo