1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi dhaifu wa Kosovo ni changamoto

18 Februari 2008

Kosovo iliyojitangazia uhuru wake kutoka Serbia siku ya Jumapili inakabiliwa na changamoto kali ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/D9N2
Kosovo Albanians celebrate with the new Kosovo flag the independence in Kosovo's capital Pristina, 17 February 2008. Kosovo's Parliament proclaimed independence from Serbia on Sunday 17 2008. Kosovo will be the 6th state carved from the Serb-dominated federation since 1991, after Slovenia, Croatia, Macedonia, Bosnia and Montenegro, and the last to escape Serbia's embrace. Kosovo has been run by the United Nations since mid-1999, after a NATO air assault drove out Serbian forces waging a brutal crackdown on separatist ethnic Albanian guerillas and their civilian supporters. EPA/ARMANDO BABANI +++(c) dpa - Bildfunk+++
Bendera mpya ya KosovoPicha: picture-alliance/ dpa

Tangu miaka na miaka Waalbania wa Kosovo wamekuwa wakigombea uhuru wao kutoka Serbia.Hatimae siku ya Jumapili,Kosovo ilijitangazia uhuru wake.Lakini eneo hilo halina msingi wa kiuchumi unaohitajiwa ili kuweza kuwa na uhuru halisi.

Kuambatana na utaratibu unaoendelea tangu mwaka mmoja kuhusu hali ya Kosovo,utaratibu huo utakapokamilika,Kosovo ingepaswa kuwa mwanachama katika Umoja wa Ulaya. Lakini viwango vya kiuchumi vikizingatiwa basi lengo hilo lipo mbali kabisa.Kwani mwaka uliopita,kwa wastani pato la kila raia mmoja wa Kosovo lilikuwa Dola 1,100 tu kwa mwaka mzima. Na pato la ndani la taifa ni sawa na Ethiopia au Zambia.

Wakati huo huo idadi ya watoto wanaozaliwa ni kubwa mno. Theluthi moja ya wakaazi milioni 2 wa Kosovo wana umri ulio chini ya miaka 14 na kila mwaka,idadi ya watu wanaotafuta ajira inaongezeka.Mtaalamu wa masuala ya kisiasa Behlul Baqaj anagutusha kuwa asilimia 50 ya Wakosovo wanakosa chakula bora na asilimia 15 hawana chakula kabisa.Kiasi ya watu 330,000 hawana ajira.Mwajiri mkubwa ni idara za serikalini na mishara mikubwa kabisa inalipwa na tume za mashirika ya kimataifa.Nusu ya biashara za kibinafsi zinahusika na biashara za rejareja na huajiri kama watu wawili au watatu tu kwa mshahara mdogo kabisa.Wengi wengine hufanya kazi za magendo na hungojea misaada ya pesa kutoka kwa ndugu wanaoishi nchi za ngámbo.Kama Waalbania wa Kosovo 375,000 wanafanya kazi Marekani, Ujerumani,Uswissi au nchi zingine zilizoendelea kiviwanda na kila mwaka,hupeleka nyumbani jumla ya kama Euro milioni 450.Hiyo ni nusu ya bajeti nzima ya Kosovo anasema mwanauchumi Ibrahim Rexhepi.Kwa maoni ya mtaalamu huyo,njia iliyokuwepo ni kufungua masoko ili kuvutia uwekezaji kutoka nchi za nje pamoja na kufunguliwa kwa mipaka ili wale wasio na ajira huko Kosovo waweze kutafuta kazi katika nchi za ngámbo kama Ujerumani au kwengineko.

Lakini nchi za Ulaya ya Magharibi zinataka kuzuia uhamiaji wa aina hiyo kutoka nchi za Balkan na badala yake hujaribu kuwavutia wawekezaji kwenda Kosovo kwa kupigia debe mishahara midogo ya eneo hilo na kodi ndogo ya mapato inayotozwa huko.Si hayo tu,Kosovo vile vile ina utajiri mkubwa wa madini kama zinki,risasi,makaa ya mawe na nikeli.

Matumaini makubwa yapo katika sekta ya nishati.Shirika la nishati la Kosovo hivi sasa huzalisha megawati 800 tu na mahitaji ya eneo hilo ni megawati 1,000.Mwaka huu mashirika ya kimataifa yatapewa mkataba wa kujenga mtambo wa tatu wa nishati.Ukitarajiwa kuwa tayari mwaka 2014,mtambo huo utazalisha megawati 2,100 kwa kutumia makaa ya mawe yaliyo karibu na kiwanda hicho cha umeme na sio kutoka eneo la kaskazini.Mitambo miwili ya zamani itafanyiwa ukarabati na mmoja utaendelea kufanya kazi kwa miaka saba mingine na wa pili utaendelea hadi mwaka 2024 na utakuwa na uwezo wa kuuza nishati katika nchi za nje. Hatua kama hizo huashiria kuwa Kosovo ndio inapiga hatua kujitegemea kiuchumi.