1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchumi wa Kenya wanawiri

Thelma Mwadzaya28 Mei 2007

Uchumi nchini Kenya unaripotiwa kukua kwa asilimia 6.1 mwaka uliopita wa 2006.Kulingana na tathmini ya kila mwaka ya kiuchumi inayofanywa na serikali uchumi umeimarika ikilinganishwa na mwaka 2005 ulipokuwa katika kima cha asilimia 5.7.

https://p.dw.com/p/CHDe
Bunge la Kenya mjini Nairobi
Bunge la Kenya mjini NairobiPicha: DW /Maya Dreyer

Uchumi wa Kenya ndio mkubwa kabisa katika eneo la Afrika Mashariki na serikali yake inatarjia ukuaji zaidi wa asilimia 5 hadi 6.5 mwaka huu.Kulingana na Waziri wa Mipango wa Kenya Henry Obwocha sekta zilizochangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji huo ni hoteli na mikahawa,biashara rejareja,usafiri na mawasiliano,ujenzi vilevile kilimo.Sekta ya Utalii inayoipa serikali fedha za kigeni iliongeza pato lake kutoka shilingi bilioni 48.9 mwaka jana hadi 56.2.

Kwa mujibu wa waziri wa Mipango Henry Obwocha Mfumko wa bei za bidhaa uliongezeka hadi asilimia 14.5 mwaka jana ikilinganishwa na asilimia 10.3 mwaka 2005.Mfumko huo wa bei ulisababishwa na bei za juu za kimataifa za mafuta vilevile ukame.Tathmini hiyo inapendekeza kuwa mfumko wa bei huenda ukapungua mwaka huu bei za chini za vyakula zikichangia vilevile mazingira yaliyostawi kiuchumi.

Tangu Rais Kibaki kuchukua hatamu za uongozi uchumi wa Kenya umeimarika kwa asilimia 2.8 mwaka 2003 na 4.8 mwaka 2994.Ukuaji wa uchumi unadhaniwa kuwa jambo litakalompa kura Rais Kibaki huku uchaguzi wa rais na wabunge ukisubiriwa mwishoni mwa mwaka.

Kulingana na wadadisi hali ya kisiasa nchini Kenya katika kipindi cha kujiandaa kwa uchaguzi huenda ikaathiri uchumi.

Wakosoaji nao wanaeleza kuwa ukuaji wa uchumi unaathiriwa na visa vya uhalifu,ufisadi na miundo msingi iliyo hafifu.Pato la serikali linatarajiwa kuongezeka hadi shilingi bilioni laki nne.

Kulingana na tathmini hiyo nafasi laki nne u nusu za kazi ziliundwa na serikali nyingi katika sekta ya kujiajiri binafsi.Uhaba wa nafasi za kazi nchini Kenya ni tatizo kubwa linalokumba serikali ya Mwai Kibaki.