1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwanini mlango ulifungwa

26 Machi 2015

Uchunguzi wa chanzo cha ajali ya ndege ya Germanwings unaendelea. Masuala kadhaa yamechomoza baada ya kufichuliwa kwamba mmojawapo wa marubani alishindwa kurejea ndani ya chumba cha rubani,baada ya kutoka hapo awali.

https://p.dw.com/p/1Exm0
Frankreich Seyne les Alpes Absturz Germanwings A320
Picha: DW/M. Luy

Katika wakati ambapo uchunguzi unawalenga marubani hao wawili,familia za wahanga wanatarajiwa kuwasili leo mchana karibu na mahala ajali hiyo ilikotokea na ambako miili ya wahanga hao imeshaanza kukusanywa.Inasemekana patahitajika siku kadhaa na pengine hata wiki kuweza kuwatambua wahanga hao,

Kwa mujibu wa duru zilizo karibu na uchunguzi,sauti za mawasiliano kutoka chumba cha marubani zilizonaswa na kisanduku kimoja cheusi kilichogunduliwa jumanne iliyopita,zinabainisha,baada ya safari kuanza kama kawaida,mmojawapo wa marubani alitoka na baadae kujikuta katika hali ya kutoweza kurejea tena,ndege hiyo ilipoanza kuteremka kwa kasi kuelekea milimani-tukio lililodumu dakika nane.

Masuala kadhaa yamezuka kuhusu marubani

"Mwanzoni,unawasikia marubani wakizungumza kama kawaida,halafu unasikia kiti kikirejeshwa nyuma,mlango unafunguliwa na kufungwa na halafu unasikia kelele za mlango unaogongwa,hakujakua na mazungumzo mpaka ndege ilipokuwa inaanguka" duru hiyo ya karibu na utafiti na ambayo jina lake halikutajwa imesema.

Deutschland Angehörige auf dem Weg zur Absturzstelle Germanwings A320
Picha: AFP/Getty Images/P. Stollarz

Marubani hao wawili walikuwa wakizungumza kwa kijerumani.Na mwishoni mwa safari,likahanikiza onyo linalobainisha ndege inakurubia ardhini-kwa mujibu wa duru hiyo ambayo haikuweza kufafanua kama aliyetoka nje ya chumba cha marubani alikuwa kamanda wa ndege au msaidizi wake.

Katika wakati ambapo ni machache tu ndio yanayojulikana kuwahuru marubani hao,shirika la ndege la Lufthansa limewaambia maripota kwamba msaidizi wa rubani ameanza kazi septemba mwaka 2013 na ameruka kwa jumla ya masaa 630.

Haijulikani pia msaidizi wa rubani ni raia wa nchi gani.

Mwendesha mashtaka wa Marseille Brice Robin aliyepewa jukumu la kusimamia ajali hii anapanga kuzungumza na waandishi habari hivi punde.Kuhusu chanzo cha ajali,kila kitu kinazingatiwa" amesema mkurugenzi wa ofisi ya uchunguzi na utafiti-BEA Rémi Jouty.

Maombolezi yanaendelea huko Haltern na Ujerumani kwa jumla

Wakati huo huo opereshini za kukusanya maiti na kutafuta kisanduku cha pili cheusi zineshaanza.Na mamia ya watu wakiwemo familia na jamaa za wahanga wameshaanza kuondoka Ujerumani na Uhispania kuelekea karibu na mahala ajali hiyo ilikotokea.Vituo viwili vya mapokezi vimefunguliwa katika kijiji cha Seyne-Les Alpes na kile cha Le Vernet.

Deutschland Schweigeminute im Bundestag Berlin Absturz Germanwings A320
Picha: Reuters/H. Hanschke

Jana viongozi wa nchi tatu,rais Francois Hollande wa Ufaransa,kansela Angela Merkel wa Ujerumani na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy walizuru eneo ajali hiyo ilikotokea.

Ujerumani na Uhispania ndizo zilizopotelewa na raia wengi katika ajali hiyo-72 wa Ujerumani na 51 wa Uhispania.

Katika mji wa kaskazini magharibi ya Ujerumani Haltern,mawardi na mishumaa imeenea katika ngazi za shule ya sekondari walikokuwa wakisoma wanafunzi 16 waliofariki katika ajali hiyo.

Jana usiku,mashabiki na wanasoka walikaa kimya dakika moja katika mechi za B ayern Munich na Real Madrid na pia katika pambano la kirafiki kati ya Ujerumani na Australia mjini Kaiserslautern.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir:AFP/Reuters

Mhariri: Josephat Charo