1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa vifo Duisburg waanza

Kabogo Grace Patricia26 Julai 2010

Vifo hivyo vilivyosababishwa na msongamano kwenye tamasha la muziki vilitokea siku ya Jumamosi katika mji wa Duisburg, Ujerumani.

https://p.dw.com/p/OUTi
Afisa wa usalama wa mji wa Duisburg, Wolfgang Rabe (kulia) na afisa wa polisi, Detlev von Schmeling, wakizungumza na waandishi habari kuhusu maafa hayo.Picha: AP

Waendesha mashitaka nchini Ujerumani, wameanza kuchunguza chanzo cha vifo vya watu 19 katika msongamano uliosababisha kukanyagana uliotokea kwenye tamasha la muziki la Love Parade katika mji wa Duisburg. Watu 342 walijeruhiwa katika msongamano huo uliotokea siku ya Jumamosi.

Akizungumza na waandishi habari katika mji wa Bayreuth, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alisema lazima uchunguzi wa kina ufanyike kubaini kilichosababisha maafa hayo.

Hapo jana gazeti la Ujerumani la Spiegel liliripoti katika mtandao wake kuwa waandalizi wa tamasha hilo walipewa kibali cha kuruhusu watu 250,000 kuhudhuria badala ya milioni 1.4 ambao walihudhuria. Mwandalizi wa tamasha hilo, Rainer Schaller alisema tamasha hilo halitafanywa tena kwa heshima ya wahanga wa maafa hayo na familia zao.