1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wafanyika kuhusu bomu Old Trafford

16 Mei 2016

Kamishna wa polisi wa mji wa Manchester ameitisha uchunguzi kuhusiana na bomu bandia lililoachwa katika uwanja wa Old Trafford baada ya zoezi la mafunzo na kusababisha kufutwa mchuano wa ligi kuu ya kandanda ya England

https://p.dw.com/p/1Iogp
Großbritannien Fußball Stadion Manchester United teilweise evakuiert
Picha: Getty Images/A. Livesy

Kifaa hicho kilisababisha watu kuondolewa katika uwanja huo wa Manchester United muda mfupi kabla ya kuanza mchuano wao wa mwisho wa msimu dhidi ya Bournemouth.

Kamishna wa Polisi wa mji wa Manchester Tom Lloyd amesema kisa hicho kilisababishan usumbufu mkubwa kwa mashabiki waliotoka sehemu za mbali kuja kutazama mpambano huo. "Nadhani klabu inapaswa kuchukua usukani kuhusu uchunguzi huu. Klabu inatambua wajibu wake. Lazima ihakikishe kuwa kuna kiwango sahihi cha uwazi utakaojitokeza utakaotuambia kuwa tunafahamu kilichotokea, tunafahamu kwa nini kikafanyika na nani anayewajibikia hilo. Lakini tunajua sasa kuwa halitafanyika tena kwa sabababu mwishowe tungetaka kulikomesha hilo.

Aidha amesema kilipoteza muda wa idadi kubwa ya polisi na kikosi cha jeshi cha watalaamu wa mabomu, na kuwaweka watu katika hatari bila sababu yoyote. Polisi ilisema kifaa hicho kilichoonekana kuwa ni bomu, ambacho baadaye kiliteguliwa kwa kulipuliwa, kiliachwa chooni kwa bahati mbaya na kampuni moja ya kibinafsi iliyokuwa inafanya zoezi la mafunzo.

Mchuano huo umepangwa kuchezwa upya hapo kesho Jumanne, lakini matumaini ya Manchester United kufuzu katika kandanda la Champions League msimu ujao ni sifuri baada ya Manchester City kumaliza katika nafasi ya nne jana kwa kutoka sare ya bao moja kwa moja na Swansea City. United pia watapambana na Crystal Palace katika fainali ya Kombe la FA siku ya Jumamosi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu