1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udugu wa kiislam waingia mafichoni

26 Agosti 2013

Msako wa polisi dhidi ya wafuasi wa Udugu wa kiislam umesababisha wengi wa wafuasi wa vuguvugu hilo kongwe la miaka 85 kurejea tena mafichoni

https://p.dw.com/p/19W5X
Maandamano dhidi ya kuachiliwa huru rais wa zamani Hosni MubarakPicha: Reuters

Mkuu wa Udugu wa kiislam,Mohammed Badie ambae kesi yake pamoja na watuhumiwa wenzake wawili,imeakhirishwa,mara baada ya kuanza kusikilizwa jana,anasemekana amepigwa na kutukanwa alipokamatwa wiki moja iliyopita.Wakati huo huo wanaharakati wa Udugu wa kiislam wameamua kuanza upya kujificha kufuatia kamata kamata nchini Misri.

Kesi ya mkuu wa Udugu wa kiislam na wasaidizi wake wawili wakuu,Khairat al Chater na Rachad Bayoumi wanaotuhumiwa kuchochea mauwaji wakati wa machafuko yaliyofuatia kuondolewa madarakani na jeshi rais aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia Mohammed Mursi imeakhirishwa hadi October 29 ijayo.

Kukamatwa Mohamed Badie,wiki moja iliyopita kumehitimisha wiki nzima ya mashambulio ya jeshi dhidi ya wafuasi wa Udugu wa kiislam ambapo zaidi ya watu 900 wameuwawa.

"Wameingia ndani ya nyumba yake,wamempiga na kumtukana matusi ya kuwakashifu mamaake na babaake" amesema wakili wake Mohammed Gharib mbele ya maripota wa shirika la habari la Uingereza Reuters.

Wakili huyo amesema mteja wake ameng'oka meno alipokamatwa na kwamba tangu alipokamatwa hapati matibabu ya maradhi yake ya mipigo ya moyo.

Kesi ya kisiasa na sio ya jinai

Kesi ya Mohammed Badie na wenzake wawili imeakhirishwa muda mfupi baada ya kuanza.Watuhumiwa wote watatu wakuu na wafuasi wengine 32 wa Udugu wa kiislam hawajakuwepo mahakamani.Afisa mmoja wa usalama anazitaja sababu za usalama kuwa chanzo cha kutofikishwa watuhumiwa hao mahakamani.

Wakili wa Chairat al Chater Atef Galal anasema kesi hii imeamuliwa hata kabla ya kuanza.Anaendelea kusema:

"Nilisema kabla kwamba hii ni kesi ya kisiasa na sio ya jinai.Ushahidi hakuna kabisa.Hizi ni shutuma zilizotungwa kudai kwamba viongozi wa udugu wa kiislam na wote wale wanaowaunga mkono wamechochea umwagaji damu.Kesi hii imeakhrishwa hadi October 29 kwasababu za usalama na watuhumiwa hawajakuwepo mahakamani,ikimaanisha uamuzi umepitishwa kabla ya kikao,hazukupitishwa leo."

Udugu wa kiislaam warejea tena mafichoni

Kutokana na kamata kamata dhidi ya wafuasi wa Udugu wa kiislam, elfu mbili kati yao wamekamatwa,wanaharakati hao hivi sasa wameamua kurejea katika hali yao ya zamani ya maisha-hawaishi tena mahala pamoja na wameanza upya kuingia mafichoni.

"Hatutumii tena mawasiliano ya simu na internet-tusije tukajulikana tuliko" amesema,mwanaharakati mmoja wa jimbo la kaskazini la Alexandria,aliyejibadilisha jina na kujiita Aicha kwasababu za usalama.

Amesema babaake ambae ni miongoni mwa wakuu wa Udugu wa kiislam ameingia mafichoni kwa hofu asije akakamatwa.

"Hali ni mbaya zaidi kuliko hata wakati wa utawala wa Mubarak" amesema mwanaharakati huyo na kuongeza tunanukuu"Mbali na matumizi ya nguvu ya polisi,kuna uhasama miongoni mwa watu.Wengi hawataki tena kuwa na majirani ambao ni wafuasi wa Udugu wa kiislam,lakini kwa bahati nzuri kuna wengine wanaotuunga mkono."Amesema Aicha.

Katika wakati ambapo kabla ya mashambulio ya jeshi ya Agosti 14 iliyopita Udugu wa kiislam uliweza kuwakusanya malaki ya wafuasi wake,hivi sasa idadi hiyo imepungua mno tangu walipogeuka lengo la hujuma za wanajeshi na polisi.

Hata hivyo baadhi ya wadadisi hawaamini kama vuguvugu la Udugu wa kiislam -lililoundwa miaka 85 iliyopita,linaweza haraka hivyo kutoweka.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu