1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udukuzi wa mtandao wa serikali wawashitua wahariri Ujerumani

Mohammed Khelef
1 Machi 2018

Suala kubwa wanaloangazia wahariri kwenye magazeti ya Ujerumani leo ni taarifa za udukuzi kwenye mifumo ya data ya serikali nchini Ujerumani unaohofiwa kufanywa na wadukuzi kutoka mataifa ya kigeni.

https://p.dw.com/p/2tVQu
Chaos Computer Club in Leipzig - CCC 2017
Picha: Getty Images/J. Schlueter

Gazeti la Berliner Zeitung linathibitisha kuarifiwa kuwa wadukuzi walikuwa wanaingilia mifumo ya mawasiliano ya serikali kuu ya Ujerumani hadi Jumatano ya jana, kwa mujibu wa vyanzo vya usalama vilivyozungumza na gazeti hilo. Mashambulizi hayo yalikuwa yakichunguzwa na maafisa wa usalama wa Ujerumani, ambao walikuwa wakijaribu kutambua malengo na utambulisho wa wadukuzi hao.

Kufikia jioni ya jana ndipo ilipobainika kwamba wadukuzi wenye mafungamano na Urusi walikuwa wameingilia mtandao wa kompyuta wa serikali ya Ujerumani. Inasemekana kuwa udukuzi huu ulitokana na kundi la ujasusi mtandaoni lijiitalo APT28, pia linalofahamika kama Fancy Bear, ambalo wachambuzi wengi wa masuala ya usalama wanasema lina mafungamano na serikali ya Urusi.

Gazeti la Suddeutsche Zeitung linaripoti kwamba mwanasiasa wa ngazi za juu wa chama cha CDU kinachoongozwa na Kansela Angela Merkel, Patrick Sensburg, ametoa wito wa kufanyika uchunguzi wa haraka juu ya suala hili.

Sensburg aliiambia kamati ya usalama ya bunge hapo jana kwamba: ikiwa data kwenye mifumo ya mawasiliano zinatoweka, maana yake ni kuwa lazima haraka pachukuliwe hatua leo kabla ya kesho. Yeye mwenyewe Sensburg ni mjumbe wa kamati hiyo ya usalama, ambayo ilipaswa kukutana kwa dharura majira ya adhuhuri jana, kuzungumzia suala hili.

Lakini wanasiasa wa upinzani wanataka hatua kubwa zaidi ya uchunguzi, wakitaka kuwajibika kwa waliopewa dhamana na hasa kwa kuzikalia taarifa hizi muhimu kwa muda mrefu.

Jared Kushner, mkwe na mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani.
Jared Kushner, mkwe na mshauri wa Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Kushner avuliwa mabawa?

Frankfurter Allgemeine linagusia taarifa ya kuondoshwa kwa baadhi ya fursa za kiulinzi na kiusalama alizokuwanazo mkwe na mshauri mkuu wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jared Kushner.

Mhariri anasema sasa Kushner yupo kweupeni kwa kuwa amenyimwa taarifa za siri za ngazi za juu. Namna Kunshner anavyojihusisha na nchi nyengine, kama vile Urusi na China, kunasemekana kuna mashaka mno kiasi cha kwamba masuala ya kiusalama bado hajayaeleweka.

Kwa hivyo, anasema mhariri, kama ilivyo kwenye serikali za kiholela, mahusiano ya kifamilia ni muhimu zaidi kuliko utaalamu kwa Trump, na kwake kila siku Kushner atasalia kuwa mshauri wake mkuu na anafurahia kufanya naye biashara. 

Mwandishi: Mohammed Khelef
Vyanzo: Frankfurter Allgemeine, Berliner Zeitung, Süddeutsche Zeitung
Mhariri: Saumu Yussuf