1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UEFA yakemea mpango wa kuanzishwa Super League

Bruce Amani
19 Aprili 2021

Kamati kuu Tendaji ya Shirikisho la Kandanda Ulaya – UEFA imekutana leo kwa mkutano wa dharura na muhimu wa kuyafanyia mageuzi mashindano ya Ligi ya Mabingwa, na kukemea mpango wa kuanzishwa Super League

https://p.dw.com/p/3sEpl
Großbritannien Schals der englischen Fußball-Premier-League-Teams
Picha: Alastair Grant/AP Photo/picture alliance

Super League ya Ulaya itashindana na Champions League kwa kuwa na mechi za katikati ya wiki zikizishirikisha timu zake 20, ambapo 15 zitakuwa za kudumu, katika msimu wa kuanzia Agosti hadi Mei. Kwanza kwa kucheza mechi 18 za awamu ya makundi na kisha za hatua ya mtoano.

Vilabu vya Manchester City na United, Arsenal, Tottenham, Chelsea na Liverpool; AC na Inter Milan za Italia pamoja na Juventus; na vitatu vya Uhispania Barcelona, Real na Atletico Madrid ndio waasisi wa ligi hiyo inayopangwa ya matajiri.

Vilabu vya Ujerumani, Bayern na Dortmund, na PSG ya Ufaransa vimepinga mpango huo. Vyama vya kandanda katika nchi vinakotokea vilabu hivyo vimepinga vikali kuundwa kwa ligi hiyo.

Vilabu hivyo 12 vimeiandikia barua UEFA na FIFA vikiyahimiza mashirikisho hayo kushiriki katika mazungumzo kuhusu mashindano hayo mapya.

Barua hiyo imesema hawataki kuchukua nafasi ya Ligi ya Mabingwa ya UEFA wala Ligi ya Europa lakini kushindana kwa pamoja na mashindano hayo.

UEFA na FIFA zimepinga kuundwa kwa mashindano pinzani na Ligi ya Mabingwa na kutishia kuviwekea vikwazo vilabu na wachezaji watakaoshiriki.

Taarifa ya vilabu hivyo imesema Kampuni ya Super League imewasilisha hoja katika mahakama husika kuhakikisha kuundwa na kutekelezwa kwa mashindano hayo wa njia shwari kwa kuzingatia sheria zinazotumika.

Champions League yatanuliwa

Hatua ya makundi ya Champions League inatarajiwa kufanyiwa mabadiliko, kwa kuongeza timu kutoka 32 hadi 36 katika kile kinachofahamika kama mfumo wa Uswisi, unaotumiwa katika mchezo wa Chess.  Ambapo vilabu vitacheza mechi 10 za makundi badala ya sita kama ilivyo kwa sasa, zote dhidi ya wapinzani tofauti.

UFEA imesema mabadiliko hayo mapya yataanza kutekelezwa mwaka wa 2024

Lengo muhimu la mageuzi haya ni kuongeza haki za matangazo kwa mashindano hayo ili kuziridhisha klabu kubwa za Ulaya zenye tamaa ya pesa na kumaliza kitisho cha kuundwa ligi mbadala.

AFP/DPA/AP/Reuters