1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa kuipa ICC ushahidi wa mauaji ya kimbari ya Cote d'Ivoire

7 Aprili 2011

Huku wapiganaji wa Alassane Ouattara wakiendelea na operesheni ya kumkamata Laurent Gbagbo, Ufaransa imesema itaikabidhi ICC nyaraka zitakazosaidia uchunguzi wa mauaji ya kimbari ya Cote d'Ivoire.

https://p.dw.com/p/10pVE
Wapiganaji wa Alassane Ouattara
Wapiganaji wa Alassane OuattaraPicha: AP

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Gerard Longuet, amesema hapo Alhamis (07.04.2011) kuwa nchi yake ina ushahidi wa eneo ambalo vikosi vyake vimekuwa vikifanya kazi ya kuwalinda raia wake, ambao unaweza kuthibitisha kiwango cha uhalifu uliofanywa dhidi ya binaadamu nchini Cote d'Ivoire.

Ingawa Longuet hakutaja kwa undani nini kilichomo kwenye nyaraka hizo, lakini vikosi vya pande zote mbili, ya Ouattara na ya Gbagbo, vinatuhumiwa kuhusika na mauaji ya maangamizi tangu mgogoro baina yao uanze kugeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe, miezi mitatu sasa.

Hapo jana, mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC), Luis Moreno-Ocampo, alisema kwamba amepanga kuanza uchunguzi juu ya tuhuma za kuwepo mauaji ya kimbari katika mji wa Duekoue, ambayo kila upande kati ya ule wa Gbagbo na wa Oauattara unamlaumu mwenzake kuhusika. Kumekuwa pia na taarifa za kugunduliwa kwa makaburi ya pamoja katika mji mkuu wa Abdijan.

Gbagbo afananishwa na Hitler

Alassane Ouattara
Alassane OuattaraPicha: dapd

Wakati hayo yakiendelea, nchini Cote d'Ivoire kwenyewe, kituo cha televisheni TCI kinachomilikiwa na upande wa Ouattara hivi leo kimeonyesha filamu inayoelezea siku za mwisho za mtawala wa zamani wa Ujerumani, Adolf Hitler, akiwa na maisha ya kuchanganyikiwa kwenye handaki lake la Berlin.

Vikosi vya Ouattara vimemzingira Gbagbo, ambaye yuko chini ya handaki mjini Abdijan, ambako amekataa kusalimu amri. Filamu hiyo ya mwaka 2004, inayoitwa Downfall, yaani Anguko, imeoneshwa ikiwa na tafsiri ya Kifaransa.

Mazungumzo yaliyokuwa yakisimamiwa na Umoja wa mataifa ya kumshawishi Gbagbo awachie madaraka na kumtambua Ouattara yamefeli, lakini mkuu wa jumuiya ya vijana wanaoumuunga mkono Ouattara, Mamadou Toure, anasema kwamba akubali asikubali, Gbagbo atang'oka tu.

"Inaweza kuendelea kwa masaa machache, lakini kwa Gbagbo jambo hili ndio limekwisha. Wote waliokuwa naye wamemkimbia: mawaziri wake, jeshi lake. Hata wale waliokuwa wakijiita vijana wake wa kizalendo sasa hawaonekani tena, kiongozi wao Charles Blé Goudé amejificha kama panya kwenye shimo lake. Gbagbo amuombe Mungu tu, lakini sifikirii kuwa Mungu anasimama na wahalifu." Anasema Toure.

Wageni waikimbia Abdijan

´Huku Gbagbo akiendelea kuzingirwa, zaidi ya wageni 1,000 wameshaukimbia mji mkuu wa Abdijan kuanzia Jumapili iliyopita. Kwa mujibu wa vikosi vya Ufaransa vilivyopo Abdijan, jana peke yake waliondoka wageni zaidi ya 300, huku wengine zaidi ya 1,500 wakiwa bado kwenye makambi ya jeshi hilo, kusubiri safari.

Raia wa Ivory Coast wakikimbia mapigano mjini Abdijan
Raia wa Ivory Coast wakikimbia mapigano mjini AbdijanPicha: Picture-alliance/dpa

Vikosi vya Ufaransa vimekuwa vikiendesha operesheni ya kuwaondosha raia wa kigeni walionasa kwenye mapigano mjini Abdijan, tangu vikosi vya Ouattara vilipoingia kwenye mji huo mwishoni mwa wiki.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Saumu Ramadhani