1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa kuondoa majeshi yake Afghanistan; mdogo wake Karzai auwawa

12 Julai 2011

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy yuko katika ziara fupi nchini Afghanistan na amesema wanajeshi 1,000 wa nchi hiyo wataondolewa kutoka Afghanistan. Wakati huo huo mdogo wake rais Hamid Karzai ameuwawa

https://p.dw.com/p/11tT5
Rais wa Ufaransa Nicolas sarkozy ambaye yuko ziarani Afghanistan.Picha: AP

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ambaye yuko ziarani nchini Afghanistan amesema kuwa nchi yake itaondoa wanajeshi 1,000 kutoka katika kikosi chake cha wanajeshi nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2012, wakati ikiharakisha uondoaji wa wanajeshi hao pamoja na Marekani. Wakati huo huo maafisa wamesema kuwa Ahmad Wali Karzai mdogo wa kiume wa rais wa Afghanistan Hamid karzai amepigwa risasi na kuuawa leo.

Rais Nicolas Sarkozy akiwa katika ziara ya saa tano ambayo haikutangazwa , ambapo atakutana na rais Hamid Karzai wa Afghanistan pamoja na jenerali David Patraeus na kukutana ba vikosi vya jeshi la Ufaransa katika jimbo la Surobi, amesema kuwa wanajeshi waliobaki wa Ufaransa watakuwa katika jimbo la Kapisa. Ufaransa ina wanajeshi 4,000 nchini Afghanistan. Tutaondoa robo ya wanajeshi hao , ambao ni wanajeshi 1,000, kati ya hivi sasa na mwishoni mwa mwaka 2012, Sarkozy amesema alipowahutubia wanajeshi wa Ufaransa katika kituo karibu na mji mkuu Kabul. Ziara ya Sarkozy inafuatia ziara ya waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta mwishoni mwa wiki na inakuja baada ya Marekani na Ufaransa kusema katika mwezi Juni kuwa zitaondoa majeshi yao mapema kuliko ilivyotarajiwa katika kampeni hiyo ya kijeshi iliyodumu sasa karibu muongo mmoja dhidi ya wapiganaji wa Taliban.

Wanajeshi wa Ufaransa wamekuwa wakihusika katika operesheni za jeshi la Marekani linaloongozwa na NATO nchini Afghanistan tangu mwaka 2001 na Ufaransa imepoteza wanajeshi 64 kutoka katika kikosi chake chenye wanajeshi 4,000, ikiwa ni pamoja na mwanajeshi aliyeuwawa jana Jumatatu kwa kupigwa risasi na mwanajeshi mwenzake katika kambi ya Kapisa.

Afghanistan Frankreich Nicolas Sarkozy in Camp Warehouse
Rais Sarkozy wa ufaransa akizungumza na wanajeshi wa kikosi cha nane cha jeshi la nchi hiyo mjini KabulPicha: AP

Kuyaondoa na mapema majeshi ya Ufaransa kutoka Afghanistan kunaweza kumuimarisha Sarkozy kabla ya uchaguzi mkuu wa rais mapema mwaka 2012, ambapo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka chama cha mrengo wa shoto kuweza kushinda kipindi cha pili. Maoni ya wapiga kura baada ya kuuwawa kwa kiongozi wa kundi la al Qaeda Osama bin Laden na majeshi ya Marekani yanaonesha kuwa zaidi ya nusu ya Wafaransa wanaunga mkono kuyaondoa majeshi hayo. Hotuba ya Sarkozy kwa wanajeshi hao inakuja siku mbili kabla ya siku ya taifa ya Bastille, ambayo inaadhimisha siku ya mapinduzi mwaka 1789 na mwaka huu sherehe hizo zitawaenzi wanajeshi waliopelekwa katika mataifa ya nje.

Wakati huo huo mtu aliyekuwa na silaha kusini mwa Afghanistan amempiga risasi na kumuua Ahmad wali Karzai , mdogo wake rais wa Afghanistan Hamid Karzai leo, wameeleza maafisa. Taarifa iliyotolewa na ofisi ya gavana wa jimbo la Kandahar imesema kuwa Ahmad Wali Karzai , ameuwawa nyumbani kwake asubuhi ya leo. Uchunguzi bado unaendelea, lakini kundi la Taliban limedai kuhusika na mauaji hayo ya mdogo wake rais wa Afghanistan, na kuliita tukio hilo kuwa ni moja kati ya mafanikio yao makubwa, katika karibu muongo mmoja wa vita. Msemaji wa Taliban Usuf Ahmad ameliambia shirika la habari la AFP kwa simu kuwa kundi hilo la wapiganaji limempa kazi hivi karibuni mtu mmoja kumuua Ahmed Wali Karzai, mtu ambaye ni mwenye nguvu lakini aliyezingirwa pia na utata katika siasa za Afghanistan.

Ahmad Wali Karzai
Mwenyekiti wa baraza la jimbo la Kandahar Ahmed Wali Karzai ambaye ameuwawa kwa kupigwa risasi leo Jumanne .Picha: AP

Akimwelezea Ahmad Wali Karzai kama mtu anayejaribu kujenga daraja kati ya makabila, Ghulam Hamidi amesema.

Kandahar ina bahati kuwa na mtu kama huyu. Anaweka uwiano baina ya makabila.

Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani amethibitisha kifo cha Karzai lakini hajathibitisha kuhusu muuaji huyo. Kuna taarifa kuwa mtu huyo aliyemuua Karzai ni rafiki na mlinzi wake binafsi, na anaaminika kumpiga risasi Karzai kwa kutumia bunduki ya AK 47.

Mwandishi . Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman