1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa na Uingereza zashuhudia ongezeko la corona

John Juma
4 Oktoba 2020

Kwa jumla watu milioni 34.84 wameambukizwa virusi vya corona ulimwenguni kote na watu milioni 1, 030,629 wameshafariki kufuatia janga hilo.

https://p.dw.com/p/3jPfL
Frankreich I Coronavirus | Menschen mit Mundschutzmasken am Eiffelturm
Picha: Kamil Zihnioglu/AP/picture-alliance

Ufaransa na Uingereza zimeweka rekodi mpya ya maambukizi ya virusi vya corona kila siku. Ufaransa imerekodi maambukizi mapya 17,000, huku Uingereza ikirekodi maambukizi 13,000 mapya.

Serikali ya Uingereza imesema ongezeko hilo la ghafla limetokana na "suala la kiufundi”

Nchini Ufaransa watu wengine 49 wamefariki ndani ya siku moja na hivyo kufanya idadi ya waliokufa kutokana na virusi hivyo kufikia 32,000 na idadi jumla ya wlaioambukizwa kufikia 606,625.

Vilabu vya pombe pamoja na migahawa imefungwa kusini mwa bandari ya Marseilles, mnamo wakati kuna hofu kuwa huenda ongezeko la maambukizi litasababisha hatua kama hizo pia zichukuliwe katika mji mkuu Paris. Kanuni za watu kuvaa barakoa hata wakiwa nje bado zinafuatwa katika miji kadhaa ya Ufaransa.

Nchini Uingereza, Wizara ya Afya imeripoti kuwa maambukizi mapya 13,000 yameripotiwa, hiyo ikiwa ongezeko maradufu ya idadi iliyoripotiwa Ijumaa. Serikali ya Uingereza imesema kuwa ongezeko hilo la ghafla la maambukizi ni kutokana na "suala la kiufundi” lililosababisha kucheleweshwa kwa kuripoti maambukizi ya awali.

India ni taifa la tatu lenye maafa makubwa kutokana na janga la corona baada ya Marekani na Brazil
India ni taifa la tatu lenye maafa makubwa kutokana na janga la corona baada ya Marekani na BrazilPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/N. Sharma

Uingereza ndiyo inaongoza kwa idadi ya vifo kutokana na virusi vya corona barani Ulaya, ikiwa imerekodi vifo 42,317. Ili kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo, serikali imeweka vikwazo kadhaa dhidi ya mikusanyiko ya watu na kuonya kuwa huenda masharti zaidi yakafuata ikiwa maambukizi hayatapungua.

India pia imerekodi maambukizi mengi mapya ya watu 75,829 ndani ya saa 24 zilizopita. Hivyo kufanya idadi ya maambukizi katika taifa hilo la bara Asia kuongezeka hadi milioni 6.5. hayo ni kwa mujibu wa data kutoka katika wizara ya Afya. Idadi ya waliokufa India kufuatia janga la COVUD-19 kufikia sasa ni takriban watu 102,000, hivyo kuwa katika nafasi ya tatu baada ya Marekani na Brazil, miongoni mwa mataifa ambayo yamerekodi idadi ya juu ya vifo.

Nchini Ujerumani, takwimu kutoka katika taasisi ya Afya ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza Robert Koch zimeonyesha kuwa idadi ya maambukizi imeongezeka kwa watu 2,279 siku ya Jumapili huku idadi watu wawili zaidi wakifa hivyo kuongeza idadi ya waliokufa kufikia 9,529

Nchini Italia, maambukizi mapya 2,844 yameripotiwa. Hilo ni ongezeko la juu zaidi kushuhudiwa nchini humo tangu mwezi Aprili wakati nchi hiyo bado ilikuwa imejifunga kufuatia vikwazo vilivyowekwa kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona.

Serikali ya Italia imetangaza kuwa mikakati ya kuzuia kuongezeka kwa maambukizi itawekwa hivi karibuni, ikiwemo kulazimisha watu kuvaa barakoa wakiwa katika maeneo ya umma.

Nchini Marekani Rais Donald Trump ambaye anaendelea kupata matibabu hospitalini baada ya kuambukizwa virusi vya corona amesema siku mbili zijazo zitakuwa muhimuzaidi kuelekea katika kupona kwake.

Kwa jumla watu milioni 34.84 wameambukizwa virusi vya corona ulimwenguni kote na watu milioni 1, 030,629 wameshafariki kufuatia janga hilo. Hayo ni kulingana na takwimu zilizojumuishwa na shirika la habari la Reuters.

Maambukizi yameripotiwa katika zaidi ya mataifa 210 tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa China Disemba 2019.

(DW)