1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa ndio mabingwa kombe la dunia 2018

Sylvia Mwehozi
16 Julai 2018

Ufaransa wametawazwa kuwa mabingwa wapya wa kombe la dunia 2018 baada ya kuwatandika Croatia mabao 4-2 katika mchezo wa fainali mjini Moscow. Hii ni mara ya pili mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1998.

https://p.dw.com/p/31VLm
Russland WM 2018 Frankreich gegen Kroatien
Picha: REUTERS

Goli la kujifunga kutoka kwa mshambuliaji wa Croatia Mario Mandzukic na penalti ya Antonie Griezman ambayo ni ya kwanza kutolewa na mwamuzi msaidizi wa vidio VAR katika fainali za kombe la dunia, kufuatia mpira aliounawa Ivan Perisic yaliifanya Ufaransa kwenda mapumziko ya kipindi cha kwanza wakiwa mbele ya mabo 2-1.

Safari ya Croatia

Taifa la Croatia lenye idadi ya watu milioni 4, kushindwa kwake kumeleta maumivu makali lakini mashabiki zake walisherehekea mafanikio ya timu yao katika historia, yanayojumuisha ushindi walioupata dhidi ya Argentina na ule wa nusu fainali dhidi ya England.

Mabao ya kipindi cha pili kutoka kwa Paul Pogba na Kylian Mbappe yaliihakikishia ushindi Ufaransa kabla ya Mandzukic kupachika bao la pili kwa upande wa Croatia kufuatia makosa yaliyofanywa na golikipa wa Ufaransa Hugo Lloris.

Russland WM 2018 Frankreich gegen Kroatien
Kutoka kulia ni rais wa FIFA Gianni Infantino, rais Vladmir Putin, rais Emmanuel Macron na rais wa Croatia Kolinda Grabar-Kitarovic Picha: Reuters/

Nahodha wa Ufaransa Lloris alinyanyua kombe la dunia wakati mvua ikinyesha katika mji mkuu wa Urusi. Kocha Deschamps wa Ufaransa aliyebebwa juu na wachezaji wake amesema"ushindi ulikuwa mkubwa na mzuri" kama ushindi wa mwaka 1998 huko Ufaransa.

"Mambo mawili ni muhimu, moja ni kwamba wachezaji hawa 23 watakuwa pamoja maisha, chochote kitakachotokea na pia kuanzia sasa hawatakuwa kama walivyo kwasababu ni ambingwa wa dunia," alisema Deschamps.

Kocha huyo ambaye alikuwa nahodha wakati Ufaransa iliponyanyua kombe la dunia 1998, amekuwa mtu wa tatu katika historia kushinda kombe hilo kama mchezaji na kocha, akiungana na Mario Zagallo wa Brazil pamoja na Franz Beckenbauer wa Ujerumani.

"Tumefanya jambo la ajabu, tumeandika historia na tutafurahia", alisema Griezman ambaye ni miongoni mwa wachezaji wa Ufaransa walioongoza kwa kupachika mabao mengi.

Rais Trump atoa pongezi

Rais Donald Trump wa Marekani ni miongoni mwa waliotuma salamu za pongezi kwa Ufaransa akisema ilikuwa "soka la ajabu" na pia amemsifu rais Vladimiri Putin wa Urusi kwa maandalizi ya michuano hiyo ambayo ameilezea kuwa "bora kuwahi kushuhudiwa".

Russland WM 2018 Frankreich gegen Kroatien
Luka Modric(kulia) mchezaji bora na Kylian Mbappe mchezaji bora chipukiziPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, aliyeonekana kushikwa na hamasa kubwa wakati mechi ikiendelea na kusimama karibu na Putin wakati wa kukabidhi kombe aliandika katika ukurasa wa Twitter "asante" kwa timu.

Putin amesema Urusi "inajivunia" kuwa  mwenyeji wa kombe la dunia, na kuongeza kwamba michuano hiyo imekuwa ya mafanikio kila nyanja.

Aliongeza kwamba wageni walio na vitambulisho vya ushabiki kwa ajili ya kombe la dunia wana pasi za bure za kuingia Urusi ndani ya mwaka huu mzima wa 2018.

Croatia walitawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa karibu asilimia 61 lakini ukuta wa walinzi wa Ufaransa haukuwaruhusu Croatia kupenya.

Mchezaji wa Croatia Luka Modric ndiye mchezaji bora wa kombe la dunia wakati Mbappe akitawazwa kuwa mchezaji bora chipukizi. Mlinda mlango wa Ubelgiji Thibaut Courtois ametangazwa kuwa golikipa bora wakati mchezaji wa England Harry Kane ameondoka na kiatu cha dhahabu kama mfungaji bora.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP