1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaachia nyaraka za mauaji ya Rwanda

8 Aprili 2015

Ufaransa imeziweka hadharani nyaraka za mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda, ambazo hadi sasa zimekuwa ni siri ya serikali. Serikali ya Rwanda imeisifu hatua hiyo, ikisema itabidi nchi hiyo iachie nyaraka zote.

https://p.dw.com/p/1F44g
Rwanda huishutumu Ufaransa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya 1994
Rwanda huishutumu Ufaransa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya 1994Picha: Getty Images

Uamuzi wa kuziondoa nyaraka hizo katika hifadhi ya siri ulitiwa saini jana mjini Paris, na unahusu nyaraka za Ikulu ya Ufaransa zilizowekwa kati ya mwaka 1990 na 1995, muda ambao unajumuisha ule wa mauaji ya kimbari ambayo yaliangamiza maisha ya watu 800,000. Chanzo kutoka ofisi ya rais Francois Hollande wa Ufaransa kimesema kwamba rais huyo alitangaza mwaka jana, kwamba Ufaransa inapaswa kuweka uwazi katika kurahisisha kumbu kumbu za wakati huo.

Ikulu ya Ufaransa imesema nyaraka hizo ambazo zimetoka kwa washauri wa kidiplomasia na kijeshi na pia katika mikutano ya wizara ya ulinzi, zitakuwa wazi kwa watafiti na mashirika ya kutetea wahanga wa mauaji yaliyofanywa wakati huo.

Rwanda yaikaribisha hatua hiyo

Waziri wa sheria wa Rwanda Johnston Busingye ambaye amenukuliwa na shirika la habari la AFP amekaribisha hatua hiyo ya Ufaransa.

''Uhusiano kati ya Rwanda na Ufaransa katika nyanja za kisiasa, kijeshi na kidiplomasia katika kipindi cha kati ya mwaka 1990 na 1995 umeghubikwa na usiri mkubwa'', amesema waziri Busingye, na kuongeza kuwa maendeleo ya hivi karibuni yatasaidia kuondoa usiri huo, na kufichua mambo ambayo hadi leo yameachwa gizani.

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: picture-alliance/dpa

''Ni matumaini yetu kwamba nyaraka hizo zote zitatolewa, na siyo sehemu tu'', amezidi kusema waziri huyo wa sheria wa Rwanda.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Mashirika yanayotetea Maslahi ya Walionusurika Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda lijulikanalo kama Ibuka, Jean Pierre Dusingizemungu, ametoa wito wa nyaraka hizo kuwekwa hadharani haraka iwezekanavyo. ''Inabidi wafanye hivyo haraka, ni hatua nzuri na ya kufurahisha''. Amesema Dusingizemungu.

Uhusiano wa kusuasua

Uhusiano kati ya Rwanda na Ufaransa umekuwa ukichechemea kwa sababu rais wa Rwanda Paul Kagame anaishutumu Ufaransa kuwa na mchango wa moja kwa moja katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, kwa sababu iliiunga mkono kwa hali na mali serikali ya wahutu wenye msimamo mkali ambayo iliyafanya mauaji hayo, yaliyolenga hasa watu ya jamii ya watutsi.

Watu zaidi ya 800,000 waliuawa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, wengi wakiwa kutoka jamii ya watutsi
Watu zaidi ya 800,000 waliuawa katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, wengi wakiwa kutoka jamii ya watutsiPicha: AP

Ufaransa kwa upande wake imekuwa ikikanusha shutuma hizo, ikisema majeshi yake yaliyopelekwa Rwanda yaliwalinda raia. Mwaka jana, Allain Juppe, waziri mkuu wa zamani wa Ufaransa ambaye wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda alikuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa rais Francois Mitterand, alisema tuhuma za Rwanda haziwezi kuvumiliwa, na alimtaka rais Hollande kufanya kile alichokiita ''kulinda heshima ya Ufaransa''. Rwanda na Ufaransa zilivunja kabisa uhusiano kati ya mwaka 2006 na 2009.

Tume ya bunge la Ufaransa iliyoundwa kuchunguza mchango wa nchi hiyo katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ilifikia uamuzi kuwa nchi hiyo haikuhusika katika mauaji dhidi ya watutsi, lakini mmoja wa makatibu wake, Bernard Cazaneuve ambaye kwa sasa ni waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, alisema nchi hiyo ilifanya makosa makubwa katika maamuzi yake.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga