1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yaishutumu NATO 'kutokufanya ya kutosha' Libya

12 Aprili 2011

Huku vita vikiendelea na jitihada za kimataifa za kuumaliza mgogoro wa Libya zikisuasua, Ufaransa imeishutumu Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwa 'kutofanya ya kutosha' kumdhibiti Gaddafi.

https://p.dw.com/p/10rn5
Ndege ya kijeshi ya Ufaransa ikiwa kwenye anga ya Libya
Ndege ya kijeshi ya Ufaransa ikiwa kwenye anga ya LibyaPicha: AP

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters, hii leo (12.04.2011)waasi wamewarudisha nyuma wapiganaji wa Muammar Gaddafi kwa umbali wa kilomita 40 kutoka mji wa Ajdabiya.

Mafanikio haya, hata hivyo, ni baada ya mapigano makali, ambayo yamesababisha upande wa waasi kupoteza, kwa uchache, wapiganaji watatu, waliouawa kwa roketi lililorushwa na vikosi vya Gaddafi kutokea eneo lililopo katikati ya Ajdabiya na Brega.

Asubuhi ya leo, waasi walionekana wakiweka vizuizi vya barabarani katika eneo la Al-Arbaeen kwenye njia ya kuelekea Brega, ikikisiwa kuwa wanajipanga kwa ajili ya kuushambulia mji huo, ambao hadi sasa umo mikononi mwa vikosi vya Gaddafi.

Ufaransa yaishutumu NATO

Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen
Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh RasmussenPicha: AP

Wakati hivyo ndivyo hali ilivyo kwenye uwanja wa mapambano, kwenye uwanja wa kisiasa kumezuka mvutano wa maneno kati ya Ufaransa na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain Juppe, ameishutumu NATO kwa kutokufanya ya kutosha kwenye operesheni ya kuzidhoofisha nguvu za kijeshi za Gaddafi.

Katika mahojiano yake ya asubuhi ya leo na kituo cha redio cha France Info, Juppe amesema bado NATO haijaonesha uwezo wake hasa mbele ya vikosi vya Gaddafi.

"NATO inapaswa kutekeleza jukumu lake kwa ukamilifu. Kwa sasa haijatimiza. Ufaransa ingelipenda kuiona NATO ikiziharibu silaha nzito za Gaddafi zinashambulia mji wa Misurata." Amesema Juppe.

Juppe ataliwasilisha suala hilo kwenye mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya, unaoanza leo mjini Luxembourg, na tena kwenye mkutano wa NATO utakaofanyika mjini Berlin kuanzia Alhamis ijayo.

Ujerumani tayari kushiriki huduma ya kibinaadamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido WesterwellePicha: picture alliance/dpa

Akiwa tayari mjini Luxembourg, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, ambaye aliongoza nchi yake kujizuia kulipigia kura Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotoa idhini ya operesheni ya kijeshi dhidi ya Libya, amesema kuwa suluhisho la kisiasa ndio njia pekee ya kumaliza mgogoro wa Libya.

Licha ya kupinga kampeni ya kijeshi, Westerwelle amesema kuwa kama nchi yake itaombwa na Umoja wa Mataifa au NATO kutoa vikosi kwa ajili ya huduma za kibanaadamu nchini Libya, itafanya hivyo.

"Hatutaki kujihusisha na vita vya Libya kabisa kabisa, lakini itakapolazimika kushiriki kwenye kusaidia matokeo mabaya ya vita hivi, kama kuwaokoa watu waliokwama, kutoa huduma za matibabu, kuwasaidia watu wanaokimbia mapigano, hapo bila ya shaka hatutatelekeza wajibu wetu." Amesema Westerwelle.

Umoja wa Afrika wataka waasi watoe mashirikiano

Wakati huo huo, Umoja wa Afrika, ambao nao umejitolea kupatanisha pande zinazozozana, umewataka waasi kutoa mashirikiano kamili kwa Umoja huo.

Hili linakuja baada ya hapo jana, Baraza la Mpito la Kitaifa, chombo cha kisiasa cha waasi, kuukataa mpango wa amani wa Umoja huo, kwa sababu haushirikishi madai yao ya msingi ya Gaddafi kuachia madaraka.

Katika taarifa yake, Umoja huo umesema kinachokwamisha kuanza kwa mazungumzo ya kutafuta amani, ni msimamo wa Baraza la Mpito kuweka madai yao hayo kuwa sharti la kuzungumza.

"Umoja wa Afrika unatoa wito kwa Baraza la Mpito kushirikiana nasi kwa maslahi makubwa zaidi ya Libya, na kusaidia utafutaji na utekelezaji wa suluhisho la kudumu na la kiadilifu la kisiasa." Imesema taarifa ya Umoja wa Afrika.

Gaddafi amekubaliana na kile kinachoitwa "ramani ya Umoja wa Afrika kuelekea kwenye amani ya Libya", lakini wachambuzi wanasema hii ni ramani isiyoelekeza kokote, kwani waasi hawauamini Umoja wa Afrika kwa sababu kadhaa, ikiwemo ile ya shutuma za mamluki wa Kiafrika kupigana upande wa Gaddafi na ukweli kwamba Gaddafi ni mfadhili mkubwa wa Umoja huo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman