1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wengi ni wakimbizi kutoka mataifa ya Afrika

Admin.WagnerD23 Novemba 2017

Ufaransa imeitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya taarifa za kuwepo kwa biashara haramu ya watumwa.

https://p.dw.com/p/2o8L9
Frankreich Präsident Macron Ankunft Felix Eboue Airport in Cayenne
Rais wa Ufaransa Emmauel Macron.Picha: picture-alliance/abaca/B. Eliot

 Rais Emmauel Macron wa Ufaransa amesema kuwauza Waafrika katika mnada, kama ilivyoripotiwa hivi karibuni na vyombo vya habari, ni uhalifu dhidi ya binaadamu, huku waziri wake wa mambo ya nje, Jean-Yves Le Drian, akiliambia bunge hapo jana kuwa serikali ya nchi hiyo imeamua kuitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili suala hilo.

"Tunafanya hivyo kama wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama. Tuna uwezo huo na tunautumia," alisema Le Drian.

Akizungumza baada ya kukutana na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Alpha Conde, mjini Paris, Rais Macron amesema amepokea kwa mshtuko taarifa ya mnada huo wa kuwauza binadamu, uliorushwa na shirika la habari la CNN, akisema ni jambo la kashfa na lisilokubalika:

"Mjadala umeanza jana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ni lazima kupata suluhisho madhubuti. Ninatumai tutaenda mbele zaidi katika mapambano dhidi ya wanaosafirisha binaadamu ambao wanafanya uhalifu huo na tutashirikiana na nchi zote ili kuuharibu mtandao huo."Amesema Macron

Wiki iliyopita, CNN ilionesha vidio ya mnada ambapo mwanaume wa Kiafrika aliuzwa kwa bei ya dola 400 kwa Mwafrika mwingine kwa ajili ya kulima.

Wengi walilalamikia vidio hiyo, akiwamo nyota wa mpira wa miguu duniani, kutoka Ivroy Coast, Didier Drogba.

Lakini Umoja wa Ulaya, nao umekosolewa kwa kushirikiana na walinzi  wa pwani wa Libya, waliotumika  kuwazuia wahamiaji.

Mapema mwezi huu, Umoja wa Mataifa ulianza kutumia sera ya Umoja wa Ulaya ya kuzisaidia mamlaka za Libya kuchunguza wahamiaji wanaojaribu kuvuuka Bahari ya Mediterranean na kuwarudisha katika jela za kutisha nchini Libya.

Libyen Flüchtlinge in Sabratha
Wakimbizi wakiwa wamejipanga msururu wakisubiri kuingia Libya, eneo la Sabratha.Picha: Reuters/H. Amara

Kiongozi wa AU akosoa ushirikiano wa nchi za Ulaya na Libya

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Guinuea, Alpha Conde, anaukosoa vikali ushirikiano huo wa nchi za Ulaya na Walibya:

"Ni hali isiyokubalika. Siyo tu kuwauza wahamiaji, lakini hata mazingira wanamoishi si ya kibinaadamu."Amesema Conde

Kiongozi huyo wa Umoja wa Afrika amesema alikuwa akiwasiliana na viongozi wote na akaongeza kuwa wanajaribu kutafuta suluhisho ikiwezekana kuwarudisha raia wao wote nyumbani.

Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Al Hussein, aliishutumu jumuiya ya kimataifa kwa kufumbia macho madhila ya kutisha wanayoyakabili wahamiaji nchini Libya.

Shirika la Habari la AFP  lilizungumza na wanaume wa Kiafrika kutoka Camerooon ambao walisema walikuwa watumwa nchini Libya, ambayo imeingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kiongozi wa nchi hiyo, Moammar  Gadhafi kuuawa mwaka 2011.

Mmoja wa wakimbizi hao 250 waliofika Cameroon siku ya Jumanne, Maxime Ndong, anasema ilikuwa ni kama jehanamu.

"Kuna biashara ya watu weusi kule. Wanaotaka watumwa wanakuja kununua," aliliambia shirika la habari la AFP, akiongeza kuwa mtu anayekataa kuuzwa utumwani, anapigwa risasi.

Mwandishi: Florence Majani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef