1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yautambua muungano wa upinzani wa Syria

14 Novemba 2012

Ufaransa imekuwa nchi ya kwanza ya Magharibi yenye nguvu, kuutambua rasmi muungano wa upinzani wa Syria, kama mwakilishi pekee wa wananchi wa Syria.

https://p.dw.com/p/16isP
Rais wa Ufaransa, Francois Hollande
Rais wa Ufaransa, Francois HollandePicha: AFP/Getty Images

Nchi nyingine za magharibi pia zimeueleza muungano hao kama hatua nzuri na kuutaka kusimamia maslahi ya makundi yote ndani ya Syria. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Paris jana usiku, Rais wa Ufaransa, Francois Hollande amesema nchi yake inautambua muungano wa kitaifa wa Syria kama serikali ya baadae ya kidemokrasia. Uungwaji mkono huo umetangazwa baada ya makundi ya wapinzani ambao walikuwa wamegawanyika kuungana dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Marekani yapongeza uamuzi wa Ufaransa

Naibu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Mark Toner amesema uamuzi wa Ufaransa ni ishara nzuri ya maendeleo. Amesema Marekani inauona muungano huo kama Mwakilishi halali wa wananchi wa Syria, lakini hatua thabiti zinahitajika kuona kweli muungano huo una uwezo wa kuwasaidia Wasyria. Mataifa ya Magharibi yamekuwa yakiwashawishi wapinzani wa Syria kuungana dhidi ya Rais Assad.

Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: Reuters

Nchi za Kiarabu na Umoja wa Ulaya waahidi kuwaunga mkono wapinzani

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya jana waliahidi kuunga mkono muungano huo wa upinzani, ambao pia umetambuliwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague ameutaka muungano huo kudhihirisha kwamba uko kwa niaba ya jamii zote za Wasyria. Hague ameelezea wasiwasi wake kuhusu mkwamo unaowekwa kwa Baraza la Usalama la umoja wa Mataifa na washirika wakuu wa Syria ambao ni Urusi na China, wanaopinga azimio la mataifa matatu ya Magharibi na yale ya Kiarabu kuhusu vikwazo dhidi ya Syria. Kwa upande wa Ujerumani, waziri wake wa mambo ya nje, Guido Westerwelle amesema nchi hiyo iko tayari kuungana na umoja wa nchi za Kiarabu kuusaidia Muungano wa Kitaifa wa Mapinduzi na Vikosi vya Upinzani wa Syria katika kumaliza mapigano. Westerwelle na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Laurent Fabius kwa pamoja wamekutana na kiongozi mpya wa muungano huo, Ahmed Moaz al-Khatib.

Human Rights Watch yatoa wito

Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch, Kenneth Roth
Mkurugenzi Mkuu wa Human Rights Watch, Kenneth RothPicha: dapd

Wakati huo huo shirika la kimataifa la haki za binaadamu la Human Rights Watch limeutaka muungano wa kitaifa wa upinzani kuheshimu haki za binaadamu na kuepuka uhalifu wa kivita. Mkurugenzi wa shirika hilo Mashariki ya Kati, Sarah Leah Whitson ametaka kipaumbele cha juu cha muungano huo kuwa kumaliza unyanyasaji unaofanywa na makundi ya wapinzani wenye silaha. Aidha, ndani ya Syria kwenyewe ndege za serikali zimeanzisha mashambulizi ya anga kwenye maeneo ya waasi kwenye mpaka na Uturuki kwa siku ya pili sasa, licha ya Uturuki kupinga hatua hiyo baada ya watu watatu kujeruhiwa. Raia 15 wameuawa katika mashambulizi kwenye miji ya Daraya na Deir Sulaiman, nje kidogo ya mji mkuu wa Damascus.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE
Mhariri: Daniel Gakuba