1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yazuwiya wakimbizi kuingia nchini mwake

Amina Mjahid
6 Septemba 2019

Uganda imetupilia mbali sera yake ya kuruhusu kila raia wa kigeni anayeomba hifadhi kama mkimbizi, ikisema baadhi ya raia hao ni wahalifu wanaokwepa mkono wa sheria huku wengine wakiwa wapinzani wa kisiasa nchini mwao

https://p.dw.com/p/3PA5z
Uganda Flüchtlinge aus DR Kongo UNHCR Camp
Picha: Reuters/J. Akena

Hapo awali ilikuwa rahisi sana kwa wakimbizi kutoka mataifa ya kigeni hasa yale jirani na Uganda na mengine yasiyo na mipaka nayo kama vile Eritrea kusajiliwa kama wakimbizi Uganda.

Lakini sasa wizara inayoshughulikia wakimbizi imetupilia mbali sera hii baada ya kubainika kuwa baadhi ya wakimbizi hao ni wahalifu wanakwepa mkono wa sheria nchini mwao na hata wakija Uganda huendeleza maovu yao.

"Sifa za wakimbizi zinazidi kuwa kizungumkuti ndio maana tumeondoa vigezo vya kuruhusu kila mtu kusajiliwa kama mkimbizi, hasa hatutaki wakimbizi kutoka nchi ambazo zimejenga uhasama na Uganda, tunasema hapana, " alisema waziri wa majanga wa Uganda mhandisi Hillary Onek.

Hivi karibuni Uganda imekosolewa na majirani zake ikiwemo Rwanda kwa kuwapa hifadhi mahasimu wa kisiasa wa utawala wa nchi hiyo, hali hii ni mojawapo ya sababu za nchi hiyo kumua kufunga mipaka yake kwa Uganda. Ijapokuwa marais wa nchi hizo mbili walisaini mkataba wa kurejesha mahusiano wiki mbili zilizopita, utekelezaji wake haujafanyika.

Wale waliosajiliwa kama wakimbizi wakutwa wakiekeza nchini Uganda

Uganda Flüchtlinge aus dem Südsudan
Picha: UNHCR/I. Kasamani

Kulingana na ripoti kadhaa za wizara ya masuala ya ndani kuna raia wengi wa kigeni ambao wamekutwa wakifanya biashara ili hali hawakusajiliwa kama wawekezaji wa kigeni ila wakimbizi. Ni makundi kama hayo ya watu ambao sasa Uganda inalenga kuzuia kuingia nchini humo wakidai kuwa wakimbizi.

Hata hivyo bila kutaja nchi, Uganda inakosoa mataifa ambayo huwatuma maafisa wake kuwakamata raia wanaotakiwa na vyombo vya sheria kuwajibikia makosa yao bila kushirikisha vyombo vya usalama vya Uganda.

Kwa upande shirika la umoja mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limefafanua kuwa halitapinga maamuzi ya Uganda ila litachangia katika kuwachuja zaidi wale wanaoomba hifadhi kama wakimbizi. "Kuna angalau watu elfu 20 ambao tunachuja kwa sasa kuhakiki kama wanastahili kusajiliwa kama wakimbizi tunafanya juhudi kukabiliana na mrundikano huo," alisema Joel Boutrou mwakilishi wa UNHCR nchini Uganda.

Idadi ya wakimbizi nchini Uganda kwa sasa inakadiriwa kuwa milioni moja laki tatu. Kulingana na takwimu angalau wakimbizi 200 huwasili Uganda kutoka mataifa ya Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan, Sudan Kusini Eritrea na kwingineko.

Mwandishi: Lubega Emmanuel/DW Kampala