1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki na Macedonia wasaini kumaliza mgogoro wa jina

Saumu Mwasimba
17 Juni 2018

Ugiriki na Macedonia zimesaini makubaliano ya awali ya kihistoria, ya kubadili jina Macedonia  na sasa itaitwa Jamhuri ya Kaskazini ya Macedonia na kumaliza mgogoro ulioharibu mahusiano ya nchi hizo tangu mwaka 1991.

https://p.dw.com/p/2ziVS
Griechenland - Die beiden Außenminister Nikos Kotzias und Nikola Dimitrov vor Alexis Tsipras und Zozan Zaev
Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Ugiriki na Macedonia zimesaini makubaliano ya awali ya kihistoria, ya kubadili jina Macedonia  na sasa itaitwa Jamhuri ya Kaskazini ya Macedonia na kumaliza mgogoro wa muda mrefu ambao umeharibu mahusiano ya nchi hizo jirani tangu mwaka 1991.

Waziri mkuu Alexis Tsipras wa Ugiriki amesema tukio hilo ni hatua ya kijasiri, kihistoria na muhimu kwa ajili ya watu wake. Naye waziri mkuu wa Macedonia Zoran Zaev, amesema nchi hizo zinapasa kuondokana  na zama za kale na kuangalia mustakabali wa baadae.

Macedonia ilipokelewa Umoja wa Mataifa mwaka 1993 chini ya jina la muda la Jamhuri ya zamani ya Yugoslavia ya Macedonia, lakini nchi zaidi ya 120 ikiwa ni pamoja na Urusi na Marekani zimekuwa zikiitambua kama nchi ya Balkan chini ya jina la Jamhuri ya Macedonia.

Polisi wa kukabiliana na vurugu waliwazuia waandamanaji wakigiriki waliokuwa wakipepea bendera kilomita kadhaa kutoka eneo la sherehe. Na katika mji wa Psarades kwa mujibu wa mwandishi wa shirika la habari la AFP mapadiri walipiga kengele katika kanisa la eneo hilo kama ishara ya kuomboleza. Makubaliano yaliyosainiwa yanalenga kuanza hatua ya kuumaliza mmoja wa migogoro  mirefu duniani  na mivutano sugu ya muda mrefu iliyoanza miaka 27 iliyopita kwa tamko la   Macedonia ilijitangazia uhuru wake lakini mizizi yake ilianzia muda mrefu toka karne zilizopita.

Griechenland - Proteste gegen das Abkommen zwischen Greichenland und Mazedonien
Picha: Reuters/A. Avramidis

Tsipras alisikika akisema kwamba wakati umefika kwa mara nyingine kuimba nyimbo za furaha katika eneo la Balkan ikiwa ni muda mfupi kabla ya waraka wa makubaliano kutiwa saini na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili. Naibu katibu mkuu anayehusika na masuala ya siasa katika Umoja wa Mataifa Rosemary DiCarlo,mjumbe wa muda mrefu wa Umoja wa Mataifa Matthew Nimetz, Mwanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini na Kamishna anayehusika na utanuzi wa Umoja wa Ulaya Johannes Hahn walikuwepo kushuhudia tukio hilo wakipiga picha kwa simu zao za Smartphones.

Baada ya kusainiwa makubaliano hayo,waziri mkuu wa Ugiriki Tsipras alivuka kwenda upande wa Macedonia wa ziwa Prespa kwa ajili ya chakula cha mchana na kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Ugiriki kuitembelea nchi hiyo jirani. Tangu mwaka 1991 serikali ya mjini Athens ilikuwa ikipinga nchi hiyo jirani kuitwa Macedonia kwasababu Ugiriki pia ina jimbo lake linaloitwa jina hilohilo la Macedonia.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri:Sylvia Mwehozi