1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki na Pegida magazetini

5 Januari 2015

Hatima ya Ugiriki katika kanda ya Euro baada ya uchaguzi, na maandamano yanayopangwa kuitishwa na wafuasi wa kundi linalopinga kuenea dini ya Kiislam barani Ulaya,Pegida mjini Cologne ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1EF2N
Mwenyekiti wa chama cha siasa kali za mrego wa shoto Alexis Tsipara (kulia)Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Hatima ya Ugiriki katika kanda ya Euro baada ya uchaguzi, na maandamano yanayopangwa kuitishwa leo usiku na wafuasi wa kundi linalopinga kuenea dini ya Kiislam barani Ulaya,Pegida mjini Cologne ni miongoni mwa yale yaliyochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanzie lakini na kizungumkuti cha Ugiriki na suala la hali itakuaje pindi wafuasi wa chama cha siasa kali ya mrengo wa kushoto wakishinda uchaguzi wa bunge na kuamua kusitisha hatua za kufunga mkaja.Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaandika:"Ikiwa baada ya uchaguzi, mazungumzo pamoja na Athens yatafikia mahala ambapo ama serikali ya Ugiriki au wafadhili watahisi wameshindwa,hapo kujitoa Ugiriki katika kanda ya Euro litakuwa suala linaloweza kuzingatiwa na ambalo kimataifa pia litakuwa na uzito mkubwa.Kwamba Umoja wa Ulaya haukubali kutiwa kishindo hilo linaweza kupewa umuhimu mkubwa zaidi kuliko maslaha ya nchi moja mwanachama.

Kansela Merkel atalazimika kuwaeleza walipa kodi

Gazeti la "Die Welt linatathmini athari za kujitoa Ugiriki katika kanda ya Euro na kuandika:"Vitisho kutoka Berlin vinabainisha sera za kutaka kuuokoa Umoja wa ulaya zimegonga mwamba.Hoja za wanaotaka kuuokoa Umoja wa ulaya "Fedha ili badala yake yafanyike mageuzi" hazifai tena.Gharama za kuiokoa Ugiriki zilizidi kuongezeka miaka ya nyuma lakini utayarifu wa Athens wa kufanya mageuzi ulizidi kupungua.Wagiriki hawako tena tayari kufuata masharti ya mageuzi ya wafadhili wa kimataifa.Zaidi ya Euro bilioni 260-kiwango ambacho ni sawa na asili mia 80 ya deni jumla la Ugiriki-wanabeba wafadhili na hasa wa nchi za kanda ya Euro.Pindi Athens ikijitoa katika kanda hiyo,sehemu ya fedha hizo zitapotea.Hapo kansela Angela Merkel atalazimika kuwaeleza walipa kodi wa Ujerumani.Tsipras na wenzake wanalijua fika hilo.

Kanisa kuu la Cologne dhidi ya Kögida

Mada nyengine iliyogonga vichwa vya habari magazetini humu nchini inahusu vuguvugu la chuki dhidi ya kile kinachoitwa "kuenea imani ya dini ya kiislam katika nchi za Ulaya":Pegida .Wafuasi wa vuguvugu hilo wamekua kila jumatatu wakifanya maandamano,kuanzia katika mji wa Dresden hadi kufikia katika miji mengine ya Ujerumani.Leo hii wamepanga kuitisha maandamano hayo katika jiji la Cologne.Wakuu wa kanisa kuu la jiji la Cologne-kitambulisho cha jiji hili ulimwenguni, wameamua kuzima taa za kanisa hilo kuanzia saa 12 magharibi hadi tatu usiku ili kubainisha upinzani wa wakaazi wa jiji hilo dhidi ya Pegida.Hata hivyo gazeti la mjini Cologne,Kölner Stadt Anzeiger linaandika :"Wajerumani wawili kati ya watano wanaonyesha angalau kuwaelewa wanaofanya maandamano hayo.Hakuna chochote kitakachoubadilisha msimamo huo.Ni ishara ya watu kupoteza imani kuelekea taasisi za jamii:vyama vya kisiasa,mashirika,kanisa na wale wote ambao wamewapa sauti zao-yaani vyombo vya habari.Kwa baadhi yao wanatosheka na ile hali tu kwamba Pegida si chama cha kisiasa kilichoota mizizi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga