1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la IMF lataka madeni yapunguzwe

25 Mei 2016

Nchi za ukanda wa sarafu ya Euro na Shirika la fedha la kimataifa zimekubaliana juu ya kuipa Ugiriki msaada mwingine wa fedha

https://p.dw.com/p/1Ity8
Viongozi wa Ukanda wa sarafu ya Euro mjini Brussels
Viongozi wa Ukanda wa sarafu ya Euro mjini BrusselsPicha: picture-alliance/AP Photo/Y. Karahalis

Mwenyekiti wa kundi la nchi zinazotumia sarafu ya Euro Jeroem Dissselbloem amethibitisha kwamba Ugiriki itapatiwa mkopo mwingine wa Euro Bilioni 10,3

Baada ya mazungumo ya karibu saa 11 mjini Brussels mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro walikubaliana kuifungulia njia Ugiriki, ya kupatiwa fedha nyingine. Kutokana na mapatano hayo Shirika la fedha la kimataifa IMF litarejea kwenye mazungumzo juu ya kuikoa Ugiriki.

Nchi hiyo inaweza kutumai kupewa kiasi cha Euro Bilioni 7.5 mnamo mwezi ujao baada ya masuala yote ya kitaalamu kukamilishwa hadi kufikia mwezi wa Julai. Ugiriki itatakiwa ilipe deni la zaidi ya Euro Bilioni 3

Nchi hiyo itapatiwa fedha hizo kwa mafungu kadhaa.

Juu ya makubaliano yaliyofikiwa mjini Brussels Mwenyekiti wa ukanda wa sarafu ya Euro Jeroem Dijsselbloem ameeleza kuwa huu ni wasaa muhimu katika mpango mrefu wa Ugiriki. Amesema ni wasaa muhimu kwa wote.

Tangu mwaka uliopita palikuwapo na hali ya kutoaminiana baina ya Ugiriki na wadai wake.

Kurejea kwa Shirika la Fedha la Kimataifa kwenye mazungumzo na Ugiriki kunatokana na wadau wote kutambua kwamba deni la Ugiriki ni kubwa sana kiasi kwamba nchi hiyo haina uwezo wa kuiingiza mapato ya kutosha ili kulipa riba.

Mkuu wa Shirika hilo tawi la Ulaya Poul Thomsen amesema wadau wametambua kuwa deni la Ugiriki halilipiki. "Tunakaribisha kuwa imetambuliwa kwamba Ugiriki inahitaji kupunguziwa madeni. Thomsen amesema ameridhika kwamba makubaliano yemefikiwa juu ya utaratibu wa kutathmini uwezo wa deni kulipika."

Mawaziri wa fedha waridhika pia

Baada ya mazungumzo yaliyofanyika hadi leo alfajiri mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro wamekubaliana kutoa fedha nyingine kwa Ugiriki kutokana na kutambua hatua kali za mageuzi zilizochukuliwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Alexis Tsipras.

Brüssel Treffen Eurogruppe Einigung zu Griechenland - Jeroen Dijsselbloem
Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Lakini hatua kubwa ni makubaliano yaliyofikiwa na nchi za Umoja wa Ulaya juu ya kuipunguzia Ugiriki madeni yake mnamo mwaka 2018 . Shirika la fedha la kimataifa wakati wote limekuwa linasisitiza juu ya Ugiriki kupunguziwa madeni yake ili iweze kujimudu kifedha.

Makubaliano yaliyofikiwa na mawaziri wa ukanda wa sarafu ya Euro ni pamoja na kuchukua hatua za muda mfupi na mrefu ili kuhakikisha kwamba Ugiriki inayalipa madeni yake.

Hatua hizo pia ni pamoja na kuipunguzia Ugiriki viwango vya riba, na kurefusha muda wa kulipa madeni.Waziri wa fedha wa Ugiriki Euclid Tsakalotos ameelezea matumaini juu ya Ugiriki, hatimaye kuweza kuondokana na kizungumkuti cha midodoro ya uchumi.

Mwandishi:Mtullya abdu./dpa, afp

Mhariri:Iddi Ssessanga