1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya Euro nchini Ugiriki

29 Juni 2015

Mzozo wa madeni ya Ugiriki na kitisho cha nchi hiyo kutoka katika kanda ya Euro ndio mada iliyohanikiza magazetini,ingawa maoni kuhusu mashambulio ya kigaidi nayo pia yamechambuliwa.

https://p.dw.com/p/1FosX
KItambulisho cha Ugiriki kutoka katika kanda ya EuroPicha: picture-alliance/dpa/A. Dedert

Tuanzie lakini na mzozo wa Ugiriki ambako wahariri wanahisi wakulaumiwa sio pekee serikali ya mjini Athens.Gazeti la "Darmstädter Echo" linaandika:"Umoja wa Ulaya umeshindwa kuushughulikia mzozo ambao,ukilinganishwa na mengine,mtu angeweza kusema ni wa kukadirika.Litakuwa kosa kuwalaumu wagiriki peke yao.Wafadhili wametumia muda mrefu kupata dawa ambayo badala ya kuiponya imeizidishia maradhi Ugiriki.Hilo lazima lijadiliwe kwa dhati barani Ulaya,na ingekuwa fursa iliyoje kwa Alexis Tsipras.Mbinu zake lakini za kimabavu hazikumsaidia badala yake zimezidi kuupanuwa ufa uliopo."

Makasha ya fedha ya Ugiriki matupu

Hofu ya kutojua kitakachotokea ndio iliyowafanya wagiriki wakimbilie kutoa akiba zao walizoweka benki.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linajiuliza kama kura ya maoni itakayoitishwa nchini humo itasaidia kubadilisha ukweli wa hali ya mambo.Gazeti linaendelea kuandika:"Kama Ugiriki,hadi kura ya maoni itakapoitishwa siku sita kutoka sasa,itajitangaza muflis,bado si dhahir.Kilicho dhahir kwa sasa ni kwamba benki zimefungwa na shughuli za fedha zitachunguzwa kwa makini.Hali inatisha na kusikitisha.Katika hali kama hiyo isiyo ya kawaida wagiriki wanatakiwa waamue kama wanataka siku za mbele kuzidi kukaza mkaja.Wananchi wanatambua makasha ya fedha ya nchi yao ni matupu.Lakini kama wastaafu,waalimu au makuli watakubali kweli kuendelea kuikaza mkaja,hilo hakuna anaeliamini.

Mashambulio ya kigaidi yachafua hadhi ya dini ya kiislam

Mada nyengine iliyohanikiza magazetini leo hii inahusu mashambulio ya kigaidi ya wanamgambo wa dola ya kiislam IS.Damu imemwagika kuanzia katika hoteli za watalii nchini Tunisia ,Lyon nchini Ufaransa hadi kufikia msikitini nchini Kuweit.Katika uhariri wake gazeti la "Frankfurter Allgemeine "linaandika:"Mamilioni ya waislam wanaishi kwa amani katika nchi za magharibi sawa na raia wa nchi nyengine wanaofuata imani tofauti.Lakini kwamba mashambulio yaliyotokea hayahusiani hata kidogo na dini yoyote,kama baraza kuu la waislam wa Ufaransa lilivyosema, si kweli, ushahidi umeonyesha na baraza hilo hilo likakiri kwamba mashambulio hayo yanachafua sifa ya dini ya kiislam.Na sio sifa tu,dini zote zinabidi ziachane na desturi fulani za kale,ili ziweze kujifungamanishe na dola inayofuata sheria na mfumo wa kidemokrasia.Nayo mataifa huru yanabidi kwa upande wao yaachane na baadhi ya ndoto mfano kuingia wahamiaji bila ya ukaguzi na kupatiwa kila mtu haki ya kuishi.Kushindwa kuivumilia nchi yako mwenyewe,wakati unamvulia adui ,huo ndio mwisho wa ustaarabu-na matokeo yake ni unyama.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga