1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yaidhinisha hatua za kubana matumizi

9 Mei 2016

Wabunge nchini Ugiriki wamepitisha mpango tata wa kupunguza malipo ya uzeeni na kupandisha kodi licha ya upinzani mkali kutoka kwa umma. Maelfu ya Wagiriki waliandamana kupinga hatua hizo

https://p.dw.com/p/1IkBg
Griechenland Athen Parlament Alexis Tsipras
Picha: picture-alliance/AP Photo/Y. Karahalis

Hatua hiyo ni ya kutimiza masharti ya wakopeshaji wa kimataifa katika jitihada za kupewa fungu jingine la fedha za mkopo zinazohitajika kuuokoa uchumi wake.

Mageuzi hayo ambayo yalipingwa na wengi, na kusababisha maandamano yaliyowahusisha maelfu ya watu jana jioni, yalipitishwa na wabunge wa chama cha serikali cha siasa za mrengo wa kushoto cha Syriza katika bunge lenye viti 300. Wabunge 153 wa Syriza na wa muungano wa Independent Greeks walipiga kura kuunga mkono mswada huo wa hatua za kubana matumizi.

Kama ilivyotarajiwa vyama vyote vya upinzani viliupinga mswada huo, ambao utapunguza malipo ya juu kabisa ya pensheni nchini Ugiriki, kuunganisha fedha za pensheni, kuongeza michango na kupandisha kodi kwa wale wenye mapato ya wastani na ya juu. Grigoris Kalomiris ni mwanachama wa bodi ya chama cha wafanyakazi wa umma

Griechenland Demonstration gegen Reformpläne
Maelfu waliandamana kupinga hatua za kubana matumiziPicha: picture alliance/dpa/A. Konstantinidis

Hayo ndiyo mageuzi ya karibuni yanayoitishwa na Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa kabla ya kutoa kitita kingine cha fedha za mkopo kutoka kwa mpango wa euro bilioni 86 wa kuuokoa uchumi wa Ugiriki uliosainiwa mwezi Julai mwaka jana, na cha tatu kutolewa kwa nchi hiyo yenye mzigo wa madeni tangu mwaka 2010.

Kura ya bunge ilikuja saa chache tu kabla ya mkutano wa dharura wa mawaziri wa fedha wa kanda ya sarafu ya euro mjini Brussels, ambao wanaharakisha kukamilisha tathmini ya kwanza ambayo imekwama kwa muda mrefu kuhusu juhudi za mageuzi nchini Ugiriki ili serikali iweze kuilipa Benki Kuu ya Ulaya mabilioni ya euro mwezi Julai mwaka huu – na kuepusha mgogoro mwingine wa kifedha katika kanda ya euro.

Waziri Mkuu Alexis Tsipras, ambaye amesema mageuzi yanahitajika ili kuuzuia mfumo wa pensheni kuporomoka katika miaka michache ijayo, aliyatetea mabadiliko hayo bungeni mapema jana, ambayo ni sehemu ya ahadi ya serikali kukusanya euro bilioni 5.4 kupitia kupunguza gharama za matumizi ifikapo mwaka wa 2018.

Kabla ya mkutano wa leo wa Brussels, wa mawaziri wa fedha wa kanda ya euro, migawanyiko baina ya wakopeshaji wenyewe imeibuka kuhusiana na mageuzi ya ziada yanayoitishwa na IMF. Mkuu wa IMF Christine Lagarde ameonya kuwa kuna “mianya mikubwa” katika mageuzi yanayopendekezwa na Ugiriki, wakati kiongozi wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Jean-Claude Juncker akisema serikali ya Athens “kimsingi imetimiza” lengo la hatua zilizoitishwa na wakopeshaji.

Kabla ya wabunge kuanza mjadala, vyama vya wafanyakazi waliojawa hasira viliandaa jana mgomo ambao ulivuruga usafiri wa umma nchini humo kwa siku ya tatu mfululizo, wakati karibu watu 26,000 wakimiminika barabarani mjini Athens na mji wa pili kwa ukubwa nchini Ugiriki, Thesaloniki kuandamana dhidi ya kupunguzwa malipo ya uzeeni na kupandisha kodi kwa wananchi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo