1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yapewa mkopo mwingine wa uokozi

Bruce Amani
16 Juni 2017

Ugiriki imeepuka kwa mara nyingine tena uwezekano wa kufilisika baada ya kufikia makubaliano na wakopeshaji wake wa Ulaya kuhusu mkopo utakaoisaidia kurejesha utulivu wa kiuchumi kwa kipindi kilichosalia mwaka huu.

https://p.dw.com/p/2emm8
Luxemburg
Picha: picture alliance/AP Photo/G. Vanden Wijngaert

Aidha, imepewa hakikisho kuwa mzigo wake wa kulipa madeni utarahisishwa wakati itakapoweza hatimaye kujisimamia baada ya karibu mwongo mmoja wa kupokea msaada wa kifedha. 

Baada ya miezi ya hali ya vuta nikuvute, ambayo ilizusha hofu ya kuongezeka tena mgogoro wa madeni nchini Ugiriki, uliodumu karibu miaka minane, mawaziri wa fedha wa nchi 19 wanachama wa kanda ya sarafu ya euro pamoja na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF, wamekubaliana jana usiku  kutolewa kwa euro bilioni 8.5 nyingine, baada ya serikali ya Ugiriki kutimiza baadhi ya mageuzi. Kupata fedha hizo lilikuwa jambo la dharura kwa sababu Ugiriki ina kiasi kikubwa cha deni la kulipa mwezi ujao wa Julai.

Luxemburg Frisches Geld für Griechenland - Eurogruppe einigt sich
Mkuu wa kundi la Euro Jeroen Dijsselbloem Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Lakini muhimu zaidi katika kipindi cha muda mrefu, kundi la mawaziri wa fedha wa kanda ya euro liliweka wazi kuwa liko tayari kuulegeza mzigo wa Ugiriki kuyalipa madeni yake wakati mpango wa sasa wa uokozi utakapokamilika mwaka ujao. Jeroen Dijsselbloem ni mkuu wa kundi la mawaziri wa fedha wa kanda ya euro "Sasa tunaingia katika mwaka wa mwisho wa kuisaidia Ugiriki kifedha. Katika kusonga mbele, tutatayarisha mkakati wa kujiondoa ili kuiwezesha Ugiriki kujisimamia yenyewe kuanzia kipindi cha mwaka ujao".

Shirika la IMF pia huenda likahusika kifedha, kwa msingi mdogo wa hadi dola bilioni mbili, lakini hilo bado linahitaji maelezo zaidi kuhusu pendekezo lililopo la kufutiwa madeni. Miongoni mwa hatua zilizopewa Ugiriki ni uwezekano wa kurefusha kwa miaka 15 deni na malipo ya riba kwa wakopeshaji wake wa Ulaya.

Christine Lagarde
Mkuu wa IMF Christine LagardePicha: Reuters/J. Naegelen

Kwa upande wake, serikali ya Ugiriki itahitaji kuendelea na nidhamu yake kubwa ya kifedha hata baada ya kumalizika kwa mpango wake wa uokozi. Wakati akikiri kuwa Ugiriki haikupata kila kitu ilichotaka, waziri wa fedha wa nchi hiyo Euclid Tsakalotos alisema nchi yake sasa ingeweza kufunua ukurasa mpya kwa kipindi chake cha mpango wa uokozi "Haya yote yaliyofikiwa leo hapa yanatupa maumaini kwamba kama Ugiriki itaheshimu ahadi zake, kama itatekeleza sera zake za maendeleo, tutakuwa katika nafasi ya kujiondoa katika mpango wa kubana matumizi mwishoni mwa mwaka wa 2018. Hivyo nna furaha leo kuliko nilivyokuwa wiki moja iliyopita"

Mojawapo ya sababu za kukwama kwan mpango wa uokozi wa Ugiriki kwa miezi kadhaa iliyopita ilikuwa ni kutoelewana kuhusu msamaha wa madeni kati ya kanda ya euro na shirika la IMF, ambalo lilichangia kifedha kwa awamu mbili za kwanza za mkopo wa Ugiriki sio ya tatu. Kabla ya kuamua kama ishiriki katika mpango wa karibuni, IMF ilitaka maelezo zaidi kuhusu hali ya muda mrefu ya deni la ugiriki Mkuu wa IMF Christine Lagarde amesema hatua za kutosha zimepigwa katika mkutano wa jana za kumwezesha kupendekeza kwa bodi ya utendaji ya IMF mjini Washington kuidhinishwa kimsingi kwa mpango wa mda wa kuiokoa Ugiriki kifedha.

Mwandishi: Bruce Amani/APE
Mhariri: Gakuba, Daniel