1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugonjwa wa Suruwa waathiri watu zaidi barani Ulaya

Josephat Charo
7 Mei 2019

Shirika la afya duniani limesema kuwa zaidi ya watu elfu 34,000 barani Ulaya walipata ugonjwa wa suruwa katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka 2019. Ujerumani sasa kuwatoza faini wazazi wasiowapeleka watoto kwa chanjo

https://p.dw.com/p/3I5ML
Schweiz Kind mit Masern
Picha: picture-alliance/KEYSTONE/U. Flueeler

Siku ya Jumanne, shirika la afya duniani lilisema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya visa vya ugonjwa wa suruwa barani Ulaya katika mwezi wa Januari na Februari mwaka huu na zaidi ya watu elfu 34 wameathirika kutokana na ugonjwa huo.

Visa vilivyorekodiwa katika nchi 421 vilisababisha vifo 13.  Idadi ya visa hivyo ilikuwa mara tatu zaidi ya visa vilivyoripotiwa katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka 2018.

Siku ya Jumanne nchini Ujerumani, maafisa wa serikali katika jimbo la kaskazini la Lower Saxony walisema kuwa mtu mmoja mzima alifariki kutokana na ugonjwa wa suruwa ijapokuwa hawakutoa umri wala jinsia ya mwaathiriwa huyo.

Shirika la afya duniani, linawahimiza maafisa wa serikali kuhakikisha kuwa watu wanaokabiliwa na hatari ya ugonjwa huo wanapata chanjo huku ugonjwa huo kwa sasa ukienea katika maeneo mengi ya dunia.

Katika taarifa, shirika hilo la afya duniani lilisema kuwa iwapo hakutakuwa na muingilio wa haraka wa kukabiliana na ugonjwa huo, virusi hivyo vitawaathiri watu wengi na kuenea katika mataifa mengi zaidi katika eneo hili na pia nje.

Chanjo ya ugonjwa wa Suruwa
Chanjo ya ugonjwa wa Suruwa Picha: picture-alliance/dpa/empics/PA Wire/O. Humphreys

"Kila fursa inapaswa kutumiwa kuwapa chanjo watoto wanaokabiliwa na athari ya kukumbwa na ugonjwa, vijana na watu wazima."

Ukraine inayokumbwa na janga la ugonjwa huo wa suruwa ilikuwa eneo la bara la Ulaya lililoathirika zaidi huku zaidi ya watu elfu 25 wakiathirika katika kipindi hicho. Romania na Albania pia zilirekodi idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa huo.

Ugonjwa wa suruwa pia unaenea katika maeneo mengine ya dunia. Visa vya maambukizi vinaongezeka nchini Marekani, Ufilipino na Thailand. Watafiti wanadai kuwa ugonjwa huo unasambaa kwa vipimo vya kutia wasiwasi kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao hawajapa chanjo katika baadhi ya maeneo.

Maafisa wa serikali wamesema kupungua kwa viwango vya chanjo kunatokana na kutokuwa na habari kuhusu chanjo hiyo ya ugonjwa wa suruwa pamoja na dhana potovu kwamba inasababisha ugonjwa wa  tawahudi.

Ugonjwa huu hatari wa Suruwa huenda ukasababisha upofu, kuharibika kwa ubongo na hata kifo.

Waziri wa afya nchini Ujerumani Jens Spahn amependekeza sheria ya kuruhusu wazazi wa watoto ambao hawajapata chanjo kutozwa faini ya hadi Euro 2500 ama Dola 2,800 huku baadhi ya visa 170 vikiripotiwa nchini Ujerumani katika miezi ya Januari na Februari.