1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhaba wa usalama unaleta uhaba wa chakula nchini Iraq

Maja Dreyer19 Februari 2007

Uhaba wa usalama nchini Iraq sasa unasababisha tatizo jingine, yaani uhaba wa vyakula. Tangu mwaka 2004, yaani baada ya kujiingiza kwa jeshi la Marekani, nchi hiyo imepata msaada wa vyakula, lakini sasa mashirika mengi yamewaondosha wafanyikazi wao kutokana na utekaji nyara nchini humo.

https://p.dw.com/p/CHlc
Kila wiki kuna habari za mashambulio ya mabomu kutoka Iraq
Kila wiki kuna habari za mashambulio ya mabomu kutoka IraqPicha: AP

"Tuangalie tu vile tunavyoomba chakula licha ya utajiri wetu." Anayesema hayo ni mzee Um Muthanna alioko mjini Baghdad. Akikaa kwenye soko la kati kati mwa Baghdad, pale ambapo akiba ya mboga si ile ya zamani, mzee huyu anavunjika moyo juu ya hali ilivyo Iraq. Anasema: "Nchi kama hiyo yenye mito miwili mikubwa ingafaa kuwa ni mtoaji mkubwa zaidi wa mboga duniani, lakini sasa inaomba chakula kutoka nchi zile zile ambazo zilisaidia kuiua."

Licha ya kuwa na ardhi nzuri ya kuvuna mboga, Iraq pia ina utajiri mkubwa wa mafuta. Lakini sasa inategemea msaada kutoka nje; na Wairaqi hawaridhiki na msaada huo, hasa msaada wa chakula, anasema mtaalamu wa kiuchumi, Bw. Jassim al-Rikabi. Anaeleza kuwa mashirika mengi yasio ya kiserikali yalianza kujihusisha nchini Iraq tangu jeshi la Marekani kuingilia nchi hiyo, lakini vyakula ambavyo vimeletwa na mashirika hayo havikuwafaa Wairaqi. Hata hivyo, iliwabidi kuvikubali kwa vile wanautegemea msaada huo.

Chini ya uvamizi, msaada mwingi wa chakula kwa Iraq ulitokea Australia au nchi nyingine zilizoiunga mkono Marekani katika vita dhidi ya Iraq. Mara nyingi lakini chakula hicho kilikuwa kibovu. Mwezi wa Julai mwaka jana wizara ya biashara ya Iraq ilikataa au iliangamiza maelfu ya tani za vyakula ambavyo vilianza kuoza.

Mtaalamu Bw. Rikabi anazilaani idara za serikali ya Iraq na za wavamizi wa Kimarekani kwa kutoweza kuhakikisha chakula kinapatikana. Anasema: "Ifikapo mwisho wa mwaka 2005 mashirika mengi ya kimataifa yaliondoka Iraq kutokana na amri za serikali zao zikihofia mashambulio dhidi ya wageni."

Hali mbaya ya usalama na uhaba wa petroli ndio pia sababu kuwa ni vigumu kwa wakulima kufikisha mazao yao sokoni. Juu ya hayo, wakulima wengi walishindwa baada ya ushuru wa forodha kwa bidhaa za kutoka nje kuanguka chini kutokana na sheria mpya iliyopitishwa na msimamizi wa zamani wa Kimarekani, Paul Bremer. Kwa hivyo, wakulima wenyeji hawakuweza kushindana na bei za chini.

Lakini bei za bidhaa za kutoka nje zimepanda sana, wakati vingi vya vyakula vinavyopatikana nchini Iraq vinatoka nchi za nje, na ukulima wa kienyeji karibu hamna kabisa tena.

Wengi wa Wairaqi bado wanategemea posho ya vyakula ya kila mwezi, mradi ambao ulianzishwa wakati Iraq iliwekewa vikwazo vya kiuchumi katika miaka ya 1990 baada ya vita vya kwanza vya Ghuba. Lakini idadi ya Wairaqi ambao hawapati posho zao inazidi kuongezeka kwa sababu ya rushwa na upendeleo kwenye njia ya kugawa vyakula hivyo.

Kulingana na wizara ya biashara, kuna aina nne tu za vyakula, yaani sukari, mchele, unga na mafuta ya kupika katika posho za vyakula. Zamani kulikuwa na vyakula vya aina 12, lakini vingine vilifutwa kutokana na kupunguzwa gharama.

"Unazungumzia posho gani", anauliza Um Jamila, mama wa watoto watano, akilalamika mbele ya waandishi wa habari. "Tumedangangwa nchi yetu nzima. Na ikiwa hali hii itaendelea hivyo kwa miezi mingine sita tutakuwa kama nchi nyingine yoyote maskini tu.”