1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri wa magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo2 Januari 2007

Hukumu ya kifo dhidi ya rais wa zamani wa Irak, Saddam Hussein na kunyongwa kwake ndiyo mada kuu iliyowashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo. Mada nyengine inahusu Ujerumani kuchukua urais wa Umoja wa Ulaya. Udondozi wa leo unaletwa kwenu na Josephat Charo.

https://p.dw.com/p/CHU5

Na tukianza na gazeti la Recklinghäuser, mhariri anasema Saddam alikufa akiilaani Marekani na kinywa chake. Ulimwengu umepumzishwa kutokana na kiongozi katili, lakini kaburi lake litakuwa mahala pa wafuasi wake kwenda kuhiji. Dikteta Saddam Hussein amekufa lakini matatizo ya Irak bado yapo. Hakuna dalili za machafuko ya kikabila na umwagikaji wa damu kumalizika hivi karibuni.

Gazeti la Fränkische Tag kutoka mjini Bamberg, linasema bila shaka Saddam alikuwa gaidi. Lakini kumnyonga haraka muda mfupi baada ya kesi yake ya kwanza kumalizika, kunazusha maswali. Serikali mpya ya Irak haikuwa na haja ya kufuata sheria katika kesi ya dikteta huyo. Njia ya kufikia demokrasia nchini Irak ni ndefu na ina vikwazo vingi mno kuliko kumnyonga dikteta.

Naye mhariri wa gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin anasema picha za video zinazoonyesha kunyongwa kwa Saddam zinaeleza janga halisi la Irak kuliko zile taarifa rasmi zilizotolewa. Kwa vile kunyongwa kwa Saddam kuliidhinishwa na serikali, kama kitendo cha kuwapoza wanamgambo wa kishia, ni vigumu mtu kuendelea kuamini kwamba serikali ya Irak bado ina haja na mdahalo na maridhiano.

Gazeti la Nürnberger Nachrichten linasema kumnyonga kwa haraka kwa Saddam ni ishara hatari ya machafuko na kulipiza kisasi inayotolewa na serikali ya waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki. Ni jambo la kushangaza kabisa kwa rais George W Bush wa Marekani kufurahia kutiwa kitanzi Saddam Hussein akikueleza kuwa hatua kubwa kuelekea demokrasia.

Mhariri wa gazeti la Mitteldeutsche la mjini Halle anasema ikiwa picha za kunyongwa Saddam zitapigwa na kuwekwa sebuleni duniani kote, yaliyotokea yatafahamika wazi. Haipaswi kusahaulika Saddam alikuwa nani. Wakati wa utawala wake alikuwa na mamlaka makubwa kiasi cha kufanya mambo kupita kiasi. Kwa Marekani ambayo inahitaji ushindi katika vita vyake dhidi ya ugaidi kunyongwa kwa Saddam si kitu cha kufurahia.

Kwamba Saddam aliyefaulu kupigana vita na Iran na aliyekuwa na nguvu anaweza kufariki kwa kutiwa kitanzi ni kejeli, limesema gazeti la Westdeutsche la mjini Düsseldorf. Nini kinachobakia? Uchochezi wa kisasi cha kumwaga damu ambao hauna uhusiano wowote na kutekelezwa kwa hukumu ya kunyongwa.

Mada ya pili inahusu Ujerumani kuchukua uongozi wa Umoja wa Ulaya wakati Bulgaria na Romania zikijiunga na umoja huo. Gazeti la Süddeutsche limeandika: Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel amesema Ulaya imefaulu pamoja. Hilo ni sawa ila kwa mipaka. Wakati mwingine baadhi ya mataifa ya Umoja wa Ulaya yanatakiwa kuchukua usukani. Umoja wa Ulaya hautakiwi kuwa na maana ya kuzisubiri nchi zinazojikokota. Ikiwa hizo ndizo zitakazoamua mwendo, basi Umoja wa Ulaya hautaweza kupiga hatua mbele.

Gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linaonya juu ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na Ujerumani kama rais wa Umoja wa Ulaya. Kutafuta malengo yake badala ya kuwa na ndoto ya kuwa taifa jipya la kusisimua barani Ulaya. Kwa mpango mzuri sera za kiuchumi na usalama ni changamoto kubwa. Kansela Merkel anatakiwa kufanya awezalo katika miezi ijayo, kuwa na msimamo pasipo kukubali kuyumbishwa. Diplomasia ya kimataifa itatatizwa na maswala ya siasa ya ndani. Kwa upande mwingine ufanisi wa sera za Umoja wa Ulaya ni ufanisi pia wa siasa ya ndani ya Ujerumani.