1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania kuandaa uchaguzi mkuu wa tatu katika miaka minne

Daniel Gakuba
15 Februari 2019

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ametangaza uchaguzi mkuu wa mapema, ambao uyumkinio utazidisha mgawanyiko katika siasa za nchi hiyo. Uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika Juni mwaka ujao wa 2020.

https://p.dw.com/p/3DTQD
Premierminister von Luxemburg  Xavier Bettel in Spanien
Waziri Mkuu Pedro Sanchez wa Uhispania Picha: picture-alliance/AA/B. Akbulut

Taarifa kwamba Wahispania watatakiwa kupiga kura tarehe 28 Aprili, huo ukiwa uchaguzi mkuu wa 3 katika kipindi cha miaka 4, zimetangazwa baada ya serikali ya kisoshalisti inayoongozwa na Waziri Mkuu Pedro Sanchez kushindwa katika kura ya bajeti iliyopigwa bungeni. Waziri Mkuu Sanchez aliipoteza kura hiyo baada ya wabunge kutoka katika jimbo la Catalonia linalotaka kujitenga, kuungana na wenzao wa upinzani kukataa bajeti ya matumizi ya serikali kwa mwaka 2019.

Katika tangazo lake la kuitisha uchaguzi mpya, Sanchez amesema hawana hata dakika moja ya kupoteza. Amesema badala ya kuendelea tu na shughuli bila bajeti ya kufanyia kazi, ni bora kuwapa nafasi Wahispania kutoa kauli yao.

''Unatarajia nini kutoka kwa serikali? unatarajia uongozi, na kufanya maamuzi, na kupitisha bajeti. Kama bajeti hiyo haipitishwi na bunge, tunawaendea wananchi wa Uhisania kuwataka watupe wingi wa kutosha bungeni, ili tuweze kushughulikia masuala ya dharura ya kijamii yaliyoahirishwa kwa miaka saba iliyopita. Ukitaka niite mtu mwenye mawazo ya kizamani, lakini bila bajeti, huwezi kuongoza.''

Zamu ya Sanchez aingia katika kisima alichomchimbia Rajoy

Madrid Parlament Pablo Iglesias Podemos Rede
Bunge la Uhispania, ambako mipango ya serikali imekuwa ikikataliwaPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Sanchez aliingia madarakani Juni mwaka jana baada ya kumwangusha mtangulizi wake, Mariano Rajoy wa chama cha Popular Party, PP katika kura ya kutokuwa na imani na serikali yake. Lakini, muungano kati ya chama chake cha kisoshalisti , vyama vinavyopinga sera ya kubana matumizi na vile vya uzalendo wa kimajimbo uliomwangusha Rajoy umesambaraika wiki iliyopita, kufuatia hatua ya Sanchez kuvunja mazungumzo na n makundi ya yanayotaka uhuru wa jimbo la Catalonia.

Kiongozi wa sasa wa chama cha kihafidhina cha PP Pablo Casado ameshangilia kipigo alichokipata Waziri Mkuu Sanchez, akimshutumu kiongozi huyo kusalimu amri kwa matakwa ya vyama vinavyotaka uhuru wa jimbo la Catalonia.

Mawimbi mapya katika bahari ya siasa za Uhispania

Uchunguzi wa maoni ya wapigakura unaonyesha hakutakuwa na mshindi wa wazi katika uchaguzi wa Aprili, hali tofauti kabisa na ilivyozoeleka katika siasa za Uhispania miongo iliyopita ambapo mojawapo ya vyama viwili vikuu kilipata ushindi.

Ingawa chama cha kisoshalisti kinaongoza kwa kiwango kidogo, upo uwezekano wa chama cha kihafidhina kuungana na chama cha Wananchi cha Ciudadanos na kukipiga kikumbo chama cha Sanchez, kama ilivyofanyika katika jimbo la Andalusia hivi karibuni.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, dpae

Mhariri:Josephat Charo