1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania yaanzisha operesheni kali dhidi ya ugaidi

Lilian Mtono
18 Agosti 2017

Uhispania imeanzisha operesheni kali dhidi ya ugaidi, baada ya mshambuliaji anayedhaniwa ni mpiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu kuvamia na lori eneo lenye watu wengi mjini Barcelona, na kuua watu 13.

https://p.dw.com/p/2iSBT
Spanien Schweigeminute nach Terroranschlag in Barcelona
Viongozi na raia mjini Barcelona wakiwa wamesimama kimya kwa muda wakiwaombea wahanga wa shambulizi Picha: Reuters/S. Perez

Uhispania imeanzisha operesheni kali ya kukabiliana na ugaidi leo hii, na kuwaua watu watano walioshukiwa kuwa walikuwa na lengo la kufanya mashambulizi mengine, baada ya mshambuliaji anayedhaniwa kuwa ni mpiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu kuvamia na lori, eneo lenye watu wengi mjini Barcelona, na kusababisha vifo vya watu 13 na kujeruhi mamia. Aidha polisi nchini humo inamshikilia mtu wa tatu anayesadikiwa kuhusika na shambulizi la kigaidi katika mji huo.

Kundi la wapiganaji linalojiita Dola la Kiislamu, IS limesema wahusika wa shambulizi hilo walikuwa wanajibu wito wake wa kuchukua hatua kwa kufanya mashambulizi kwenye mtaa maarufu wenye shughuli nyingi mjini Barcelona, ambao ulikuwa umefurika watalii.

Aidha, kiongozi wa mkoa wa Catalonia Charles Puigdemont ameonya leo hii kwamba kuna mtuhumiwa aliyekuwa akipanga mashambilizi mengine mawili katika mji wa Barcelona na mji mwingine maarufu ulioko pembezoni mwa bahari akisema bado anaweza kusalia kuwa kitisho. 

Mshambuliaji alivamia eneo la biashara mjini Barcelona, ambalo ni maarufu kwa kutembelewa na idadi kubwa ya raia na watalii, na kuua na kujeruhi raia kutoka angalau mataifa 20 tofauti, mamlaka za mkoa wa Catalonia zimearifu. Haikuwa wazi iwapo mtu aliyemakatwa alikuwa ni dereva wa lori, ambaye alikimbia baada ya kuvamia eneo hilo lenye shughuli nyingi la Las Ramblas, jioni ya jana, alhamisi.

Mkuu wa Polisi wa Catalonia Joseph Lluis Trapero amesema wawili ya waliokamatwa ni raia wa Morocco na mmoja raia wa Uhispania anayetokea eneo la Mellila lililopo Kaskazini mwa Afrika linalomilikiwa na Uhispania. Miongoni mwao hakuna aliyebainika kuwa na mahusiano na ugaidi hapo nyuma. 

Spanien Polizeipräsenz am Tag nach dem Terroranschlag in Barcelona
Kumeongezwa hatua za kiulinzi hususan katika mji wa Pwani.Picha: Reuters/S. Perez

Kundi la wapiganaji linalojiita Dola la Kiislamu IS, limearifu kupitia mtadao wake wa propaganda wa Amaq kwamba wapiganaji wao walihusika na shambulizi hilo.

Saa kadhaa baada ya tukio hilo, polisi walisema waliwaua watu watano wanaoshukiwa kuwa magaidi waliojaribu kuwakanyaga watembea kwa miguu katika mji wa Cambrils ulioko Catalan, Kilomita 100, Kusini-Magharibi mwa Barcelona.

Taarifa za kipolisi kupitia ukurasa wa Twitter zimesema, washukiwa hao walikuwa wamevalia mikanda yenye vilipuzi bandia.

Kumetangazwa siku tatu za maombolezo nchini Uhispania na muda wa kukaa kimya itakapofika majira ya mchana huko Barcelona, wakati ambapo kumechukuliwa hatua za kuimarisha ulinzi katika mji wa pwani.
   

Ufaransa imesema, raia wake 26 wamejeruhiwa, 11 miongoni mwao wakiwa na hali mbaya sana. Ubelgiji yenyewe imesema raia wake mmoja, ni miongoni mwa waliouawa. Shirika la utangazaji la Ujerumani, ZDF limearifu raia wake watatu waliuawa, lakini serikali mjini Berlini bado haijasema lolote kuthibitisha taarifa hizi.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Iddi Ssessanga