1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uholanzi na Uruguay kuwania kuingia fainali ya kombe la dunia leo

Sekione Kitojo6 Julai 2010

Uruguay na Argentina zitashuka dimbani leo kuwania nafasi ya kukata tikiti ya fainali ya kombe la dunia mwaka huu 2010.

https://p.dw.com/p/OBYk
Kocha wa Uholanzi Bert van Marwijk akizungumza na waandishi wa habari kabla ya pambano la leo kati ya Uholanzi na Uruguay.Picha: AP

Leo  ni  leo atakayesema  kesho  muongo, ndivyo wasemavyo  Waswahili. Leo  ni  mwanzo  wa  michezo  ya nusu  fainali  za  kwanza  katika   kinyang'anyiro  hiki  cha kombe  la  dunia,  huko  Afrika  kusini.  Timu zinazoteremka  uwanjani  hii  leo  kuwania  tikiti  ya kucheza  katika  fainali  ni  Uruguay   na  Uholanzi. Sekione Kitojo  anatupasha   mengi  zaidi  kuhusu  mchezo  huo unaosubiriwa  kwa  hamu  na  wapenzi  wa  kandanda duniani.

Wachezaji  wa  Uholanzi  wameonywa  kutovimba  vichwa na  kutokuwa  na  dharau  wakati  watakapoteremka uwanjani  kupambana  na  Uruguay  katika   mchezo  wa kwanza  hii  leo  wa  nusu  fainali, wakati  Argentina  na Brazil  wanaendelea  kutafakari  kile  kilichowakuta  na kuondolewa  katika  kinyang'anyiro  cha  mwaka  huu  cha fainali  za  kombe  la  dunia.

Wachezaji  wawili  wa  Uholanzi  Wesley Sneijder  na  Arjen Robben  wanakutana  uso  kwa  uso  na  nyota   kutoka Uruguay  Diego  Forlan  leo  usiku, wakati  David  Villa   wa Hispania   na  Miroslav  Klose  wa  Ujerumani wataoneshana  nani  mbabe   wa  kuufumania  nyavu  hapo kesho  katika  nusu  fainali  nyingine.

Holland   haijaweza  kuonyesha  kandanda  lao  safi lililozoeleka la  pasi  maridadi  katika  fainali  hizi   huko Afrika  kusini, lakini  kocha  wao  Bert van Marwijk amesisitiza   kuwa  timu  yake   haionyeshi  ishara  za majivuno  ambayo  huwa  ni  kawaida  yao  huko  nyuma.

Siwezi  kubadilisha  utamaduni,  lakini  nimefanya kazi ngumu  kuweza  kuweka   mazingira  ya  kuwafanya wachezaji  watambue kuwa  iwapo  wanataka   kupata mafanikio   mashindanoni, ni  lazima  wautafakari  mara zote    mchezo  ujao, amesema  van Marwijk, ambaye kikosi  chake  kinakabiliana  na  Uruguay  ambayo imepungua  uwezo  wake.

Nchini  Brazil  Luiz Felipe  Scolari  anaripotiwa  kuwa anaongoza  katika  orodha  ya  makocha  wanaotarajiwa kuchukua  wadhifa  wa  kuifundisha  timu  hiyo  baada  ya kuondoka  kwa  Dunga. Orodha  hiyo  ni  pamoja  na  Mano Menezes, Muricy Ramalho, Ricardo Gomes  na   kocha  wa zamani  wa  AC Milan Leonardo.

Nchini  Argentina  taarifa  zinasema  kuwa  rais  wa shirikisho  la  kandanda  nchini  humo  Julio Grondona, amesema  kuwa  Maradona  anaweza  kuamua  mwenyewe hatima  yake, kuendelea  ama  kuacha  kuifundisha  timu ya  taifa  ya  Argentina.

Wakati  huo  huo serikali  ya  Nigeria   imesema  jana kuwa  hatua  ya  marufuku  ya  miaka  miwili , iliyowekwa dhidi  ya  timu  ya  taifa  hilo  baada  ya  kuonyesha mchezo  dhaifu  katika  mashindano  ya  kombe  la  dunia nchini  Afrika  kusini  imeondolewa. Rais  wa  nchi  hiyo Goodluck  Jonathan  alichukua  hatua   hiyo  wiki  iliyopita baada  ya  kuzuka  hasira  katika  taifa  hilo  la  Afrika  ya magharibi  baada  ya  Super Eagles  kufanikiwa  kupata point  moja  tu  kutokana  na  michezo  mitatu  katika  moja kati  ya  makundi   rahisi  katika  duru  ya  kwanza.

Shirikisho  la  kandanda  duniani  FIFA ,  liliitaka  Nigeria kuondoa  marufuku  hiyo  hadi  Jana   Jumatatu  la  sivyo shirikisho  la  kandanda  la  Nigeria  litasimamishwa uanachama  wake  katika  shirikisho  hilo  la  dunia, na kuiondoa  kabisa  nchi  hiyo  kutoka  katika  michezo  yote ya  kimataifa, kikanda  na  barani  Afrika.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / AFPE

Mhariri:Mwadzaya,Thelma