1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza haitabadilisha msimamo kuhusu Brexit

Yusra Buwayhid
30 Novemba 2020

Uingereza na Umoja wa Ulaya zimepeana tahadhari kwamba muda unayoyoma kwa pande hizo mbili kuafikiana juu ya makubaliano yao ya kibiashara kufuatia mchakato wa Brexit wa Uingereza kujitoa katika umoja huo.

https://p.dw.com/p/3m1t6
England | Fortsetzung Gespräche Brexit-Handelspakt in London | Michel Barnier
Picha: Victoria Jones/dpa/picture alliance

Masuala muhimu yaliyosalia bila ufumbuzi ni pamoja na haki za uvuvi, misaada ya serikali kwa makampuni ya biashara na sheria za kutatua mizozo kati ya pande hizo mbili. 

Soma pia: Umoja wa Ulaya, Uingereza zarejea kwenye meza ya mazungumzo

Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema leo kwamba nchi yake inataka kufikia makubaliano ya kibiashara na Umoja wa Ulaya haraka iwezekanavyo, lakini haiko tayari kubadilisha msimamo wake katika mazungumzo hayo.

Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yakiwa yanaendelea, waziri wa Mazingira wa Uingereza George Eustice amesema ana matumaini makubwa kwamba makubaliano yaweza kufikiwa. Lakini pia alikiri kwamba vizuizi kadhaa bado vimesalia.

"Umoja wa Ulaya utahitaji kubadilisha msimamo wake ikiwa unataka kufikia makubaliano, kwa kuwa tunachoomba katika suala la uvuvi ni kupewa haki sawa na zile ilizonazo Norway, na lengine tunaloomba ni kuwa na sheria zetu katika kutoa misaada ya serikali, na hayo kwetu ni maombi yenye busara.”

Johnson stimmt Großbritannien auf harten Bruch mit EU ein
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Downing Street/PA/dpa/picture-alliance

Uingereza inaondoka katika Umoja wa Ulaya mnamo Desemba 31, pale kipindi cha mpito cha uanachama usio rasmi kitakapomalizika.

Taifa hilo lilijitoa rasmi Januari mwaka uliopita, na tangu wakati huo pande hizo mbili zimekuwa zikijaribu kusaka makubaliano ya kibiashara yenye thamani ya takriban dola trilioni moja kila mwaka.

Waziri Mkuu Boris Johnson, ambaye pia kwa wakati huu anakabiliwa na kibarua kigumu cha kupambana na idadi kubwa ya vifo barani Ulaya vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19, amesema itakuwa vyema ukipatikana mpango huo lakini Uingereza, ambayo ilijiunga na Umoja wa Ulaya mnamo 1973, haina ulazima nao.

Chanzo kimoja kutoka upande wa Umoja wa Ulaya kimesema mazungumzo yalikuwa magumu mno mwishoni mwa wikiendi iliyopita, na kwamba bado kuna tofauti kubwa kati yao kuhusu masuala muhimu ya haki za uvuvi, haki za ushindani wa kibiashara pamoja na sheria zitakazolinda jinsi ya kumaliza mizozo kati ya pande hizo mbili baada ya Uingereza kutoka kabisa kwenye umoja huo.

Kushindwa kupatikana makubaliano hayo kutaleta usumbufu kwenye mipaka, kutatishia masoko ya biashara na kuvuruga usambazaji wa bidhaa kote barani Ulaya na kwengineko. Na hilo litakuwa na athari zaidi katika wakati huu amabpo ulimwengu mzima unapambana na janga la maambukizi ya virusi vya corona