1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kuwasilisha azimio kuhusu Syria

Admin.WagnerD28 Agosti 2013

Uingereza inatarajiwa kuwasilisha azimio kuihusu Syria kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo huku wachunguzi wa umoja huo wakiwasili katika ngome ya waasi viungani mwa Damascus kuendesha uchunguzi.

https://p.dw.com/p/19XoZ
Picha: Getty Images/Afp/Carl Court

Marekani na washirika wake zinajitayarisha kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Syria kutokana na madai ya kutumika kwa silaha za kemikali. Uingereza inatarajiwa kuwasilisha azimio kuihusu Syria kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo.

Huku hayo yakijiri, kundi la wachunguzi wa Umoja wa mataifa wamewasili katika ngome za waasi kuanza uchunguzi wao.

Kwa mara ya kwanza tangu shambulizi linaloaminika kuwa la silaha za sumu karibu na mji mkuu wa Syria Damascus lililowauawa mamia ya watu, Marekani imeonyesha wazi kuwa itachukua hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Syria baada ya makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden kusema kuwa shambulio hilo haliwezi kuwa lilifanywa na mwingine ile majeshi ya Rais Bashar al Assad.

Marekani kuishambulia Syria hata kesho

Uingereza pia imesema ni utawala wa Syria uliohusika katika shambulio hilo na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema nchi yake na washirika wake inatafakari iwapo hatua za kijeshi zinahitajika kuzuia na kukomesha matumizi ya silaha za kemikali katika siku za usoni.

Wachunguzi wa umoja wa Mataifa wakielekea katika eneo linaloshukiwa kushambuliwa kwa silaha za kemikali
Wachunguzi wa umoja wa Mataifa wakielekea katika eneo linaloshukiwa kushambuliwa kwa silaha za kemikaliPicha: picture-alliance/dpa

Maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani wamesema huenda jeshi la nchi hiyo likaishambulia Syria hata kesho.Huku nchi za magharibi zikiwa karibu kuishambulia Syria,wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamezuru eneo linalioshukiwa kushambuliwa kwa silaha hizo za sumu viungani mwa Damascus leo na kuanza mara moja uchunguzi wao kwa siku ya pili sasa.

Wachunguzi hao wanaosindikizwa na waasi wamewasili katika mji wa Maleiha na wataelekea katika miji iliyoathirika kuendesha uchunguzi wao.Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon amesema wachunguzi hao wanapaswa kupewa muda kubaini iwapo silaha hizo zilitumika katika vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe.

Suluhisho la kidiplomasia linahitajika

Akizungumzia shambulio hilo, Ban amesema kilichoshuhidiwa hakijawahi onekana tena katika karne hii ya 21 na kwamba ni muhimu kwa wachunguzi hao kuachwa kufanya kazi yao bila muingilio wowote na tayari wameshakusanya ushahidi muhimu na kuwahoji wathiriwa na walioshuhudia na kutoa wito kwa suluhisho la kidiplomasia kupatikana katika mzozo huo wa Syria.

Mwanamume wa Syria akimuondoa mtoto kutoka moshi mkubwa
Mwanamume wa Syria akimuondoa mtoto kutoka moshi mkubwaPicha: Bulent Kilic/AFP/Getty Images

Waziri mkuu wa Uingereza amesema azimio kuhusu Syria linatarajiwa kuwasilishwa katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa baadaye hii leo.

Kwa mara nyingine tena Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa Assad imeonya kuwa shambulio dhidi ya Syria itayumbisha kanda nzima ya Mashariki ya kati na wanadiplomasia wa Syria katika umoja wa Mataifa wamewalaumu waasi kwa shambulio hilo la kemikali ili kuchochea hatua za kijeshi kutoka jamii ya kimataifa.

Urusi imewaondoa raia wake 116 na raia wa nchi nyingine za iliyokuwa Soviet kwa ndege mbili za wizara ya kushughulikia mikasa ya dharura ambayo iliwabeba kutoka mji wa bandarini wa Latakia.Hatua hii ni kufuatia hofu kuwa Marekani na washirika wake huenda wakaishambulia Syria wakati wowote.

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema Iwapo Marekani itaishambulia Syria itakuwa janga kubwa kwa kanda hiyo na kulinganisha eneo hilo la mashariki ya kati na bomu linalosubiri kutufuliwa huku hali yake ya baadaye isiweze kutabirika.

Naye askofu mkuu wa kianglikana nchini Uingereza Justin Welby amemtaka Cameron kutochukua hatua kwa pupa akionya hatua ya kijeshi dhidi ya Syria huenda ikawa na athari ambazo hazikutarajiwa katika nchi za kiislamu.Huku waziri mkuu wa Israel akiitisha kikao cha baraza la mawaziri kuijadili Syria.

Mwandishi.afp/reuters/ap

Mhariri: Josephat Charo