1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza na Ubelgiji zalalamikiwa kwa machafuko ya DRC

Eva Klaue-Machangu21 Julai 2009

Shirika lilisilo la kiserikali linalojihusha na haki za kibiniadamu la Global Witness limetoa wito kwa serikali za Uingereza na Ubeligiji kufanya jitihada za ziada kupumaliza machafuko nchini DRC.

https://p.dw.com/p/IuU6
Wakimbizi wakiyahama makazi yao nchini DRCPicha: AP

Shirika lilisilo la kiserikali linalojihusha na haki za kibiniadamu la Global Witness limetoa wito kwa serikali ya mataifa kadhaa zikiwemo za Uingereza na Ubelgiji kufanya jitihada za ziada kuyadhibiti makampuni yanayonunua madini kwa wafanyabiashara wanaotoa silaha kwa vikundi vya Waasi katika nchi ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London,Uingereza serikali zinazohusika katika biashara ya madini nchini DRC zimeshindwa kutatua mgogoro nchini humo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 12 sasa.

Global Witness imeyashutumu makampuni ya Thailand Smelting na Refining Co,Kampuni ya Chuma ya Uingereza AMC na kampuni ya Kibelgiji kwa kuchochea migogoro nchini humo.

Migodi mingi ya madini huko mashariki ya Congo inadhibitiwa na vikundi vya waasi na jeshi la serikali na kuendeleza unyonyaji wa hali ya juu kwa wananchi wa kawaida.

Miongoni mwa madini ambayo yanapatikana katika migodi hiyo ni shaba, chuma, dhahabu na mengine ya cassiterite na coltan ambayo yanatumika kutengenezea vifaa kama simu za mkononi, kompyuta na vifaa vingine vya umeme.

Makampuni husika yanafahamu kwamba wanaowauzia madini hayo wanahusika na vitendo vya kuwapa silaha vikundi vya waasi.

Ripoti ya Global Witness mara hii imelenga katika maeneo ya DRC mashariki ambapo vikundi mbalimbali vya waasi na majeshi ya serikali yanadhibiti sehemu kubwa ya biashara ya madini.

Ripoti hii imeeleza kuwa adha hiyo imesababisha zaidi ya watu laki moja kuyakimbia makazi yao katika miezi ya hivi karibuni na zaidi kutokea matukio ya mauji, ubakaji na hata katika maeneo ya Kaskazini na Jimbo la Kivu ya Kusini.

Kämpfe im Kongo
Wanajeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya CongoPicha: AP

Ripoti imeyatuhumu makampuni hayo ya nchi za Magharibi, likiwemo la Thaisarco, kwa mtiririko mbaya wa upataji madini hayo ambao unaleta athari kwa umma.

Aidha Global Witness imetaka Umoja wa Mataifa uweke vikwazo kwa makampuni husika ili kuweza kukomesha vitendo hivyo.

Ripoti hiyo imenukuu makubaliano yatokanayo na Umoja wa Mataifa yanayoeleza kuwa "yeyote anaetoa silaha kwa vikundi vya waasi kwa ajili ya kujinufaisha kwa rasilimali ya DRC atawekewa vikwazo, vikiwemo vya kuzuiwa kusafiri na kuzuiliwa mali zake."

Shirika hilo la Global Witness limeendelea kusisitiza kuwa baadhi ya makumpuni yanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, lakini wasambazaji wao wanakusanya madini kwa kutumia vikosi vya waasi na majeshi.

Kampuni ya Madini ya Kiingereza-AMC- pamoja na kukanusha vikali madai hayo, imesema imeanza kuhakiki vyanzo vyake vya kupokea madini tangu Julai mosi mwaka huu.

Takwimu za hivi karibuni za Benk ya Dunia zinaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 10 wanategemea madini nchini DRC.


Mwandishi-Sudi Mnette AFPE

Mhariri-Miraji Othman