1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza na Ufaransa zakutana kabla ya mkutano wa G8

Kabogo Grace Patricia6 Julai 2009

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown akutana na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa ikiwa ni siku mbili kabla ya mkutano wa G8

https://p.dw.com/p/IhzY
Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, (shoto), akisalimiana na Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown.Picha: AP

Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ameungana na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa katika mji uliopo kwenye milima ya Alps kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa nchi zilizoendelea kiviwanda duniani G8 na kukubaliana kuhusu juhudi mpya za kuzuia wimbi la wahamiaji wanaoingia Ulaya. Mkutano huo wa G8 utafanyika nchini Italia kuanzia Julai 8 hadi 10, mwaka huu.

Mkutano huo wa 30 baina ya Ufaransa na Uingereza unafuatia ziara ya kitaifa iliyofanywa na Rais Sarkozy mjini London mwezi Machi, mwaka uliopita, wakati Bwana Brown alipotangaza kuwa uhusiano baina ya nchi hizo ulikuwa ukiongezeka. Mkutano huo unafanyika siku mbili kabla ya mkutano wa viongozi wa G8 utakaofanyika katika mji wa L'Aquila nchini Italia, na unazungumzia kuhusu matatizo ya ulimwengu, likiwemo suala la mabadiliko ya hali ya hewa na mgogoro wa Iran.


Marais hao wa Ufaransa na Uingereza wanatarajia kutoa wito wa pamoja kwa G8 kuchukua hatua za kupunguza uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira, kusimamisha bei ya mafuta isiyotabirika na kuangalia kwa karibu mabenki baada ya msukosuko wa kiuchumi ulioikumba dunia mwaka uliopita.


Aidha, maafisa wa Ufaransa wamesema kuwa nchi hizo mbili zitasaini makubaliano ya kuimarisha udhibiti wa uhamiaji kwa ukanda wa pande zote kwa kuongeza doria na kuwajibika zaidi katika kuongeza rasilimali.


Mpango huo utaisaidia serikali ya Rais Sarkozy kutimiza ahadi yake ya kufunga kambi iliyovamiwa bila ruhusa iliyoko kaskazini mwa nchi hiyo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, iliyokuwa ikitumiwa kama njia kuu ya wahamiaji wanaojaribu kuingia nchini Uingereza.


Kwa muda mrefu Ufaransa imeiomba Uingereza kuisaidia kutatua tatizo la wahamiaji katika bandari ya Calais, ambako mamia yao wanaoomba hifadhi wanaishi katika mahema wakijaribu kudandia malori yanayovuka Ukanda huo kwa njia ya meli au treni.


Kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, Sarkozy na Brown wanatarajia kuwa na msimamo wa pamoja na kuwataka viongozi wenzao wa G8 kuongeza shinikizo ili mpango wa kupunguza uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira ufikiwe katika mkutano ujao wa mwezi Desemba utakaofanyika mjini Copenhagen.


Nchi 27 za Umoja wa Ulaya zimekubaliana kupunguza uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2020, namba inayoweza kuongezeka hadi asilimia 30 ikiwa nchi hizo zitatekeleza mpango huo.


Viongozi hao kwa pamoja wamekuwa wakifanya kazi kuhakikisha nchi zao haziyumbi kutokana na msukosuko wa kiuchumi, ambao umesababisha kudorora kwa uchumi wa nchi hizo mbili na nchi nyingi za Ulaya.


Katika hatua nyingine viongozi hao wawili watajadili mradi wa baadae wa euro bilioni 20 wa kujenga ndege ya kijeshi chapa Airbus A400M, ambao umekuwa ukichelewa.


Mwandishi: Kabogo, Grace Patricia (AFP)


Mhariri: M. Abdul-Rahman